Uhuru ashtumiwa kwa kupanga njama kumfurusha Ruto

Muhtasari

• Washirika wa Ruto wamemshutumu Rais Kenyatta kwa kuongoza njama ya kumlazimisha  Ruto kujiuzulu kutoka serikalini.

• Madai haya yanajiri wiki moja  baada ya Rais Kenyatta kumtosa Ruto aondoke serikalini ikiwa hajaridhika.

Naibu rais William Ruto na wabunge wa mrengo wa Tanga Tanga nyumbani kwake mtaa wa Karen, Nairobi.
Naibu rais William Ruto na wabunge wa mrengo wa Tanga Tanga nyumbani kwake mtaa wa Karen, Nairobi.

Taarifa ya James Mbaka 

 

Washirika wa Naibu Rais William Ruto wamemshutumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kuongoza njama ya kumlazimisha naibu wake kujiuzulu kutoka serikalini.

 

Wandani hao wa Ruto walidai kuwa wanajua mpango wa kumfanya naibu rais asifanye kazi yoyote kwa kumpa mtu mwingine majukumu yake.

Naibu rais siku ya Jumamosi aliibua mjadala mkali nchini wakati alidai kwamba, licha ya mchango wake katika ushindi wa Uhuru mwaka 2013 na 2017, mpango ulikuwa ukiendelea wa kumtoa nje ya serikali.

"Kuna watu wanafanya njama za kunisukuma nje ya serikali. Wakati tunaunda serikali hii, Rais Kenyatta alikuwa pamoja nami au na viongozi wa kisiasa ambao wako naye?" Ruto aliuliza umati huko Kabarnet Jumamosi.

Matamshi yake yalijiri wiki moja tu baada ya Rais Kenyatta kumtosa aondoke serikalini ikiwa hajaridhika.

 

Siku ya Jumapili, Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua aliiambia gazeti la Star kwamba wanafahamu mpango wa kuunda ofisi yenye nguvu katika ofisi ya Rais kwa nia ya kumfanya Ruto asiwe na maana serikalini.

Mbunge huyo alitaja kile alisema ni  serikali kudharau wazi sheria na maswala mengine mengi kama ishara tosha kuwepo kwa njama ya kumfurusha naibu rais "chochote kinawezekana katika utawala wa Uhuru" kwenda mbele.

"Tunaishi katika nchi hii na tumeona kinachoendelea na kwa hivyo tunajua chochote kinawezekana ikiwa ni pamoja na kuunda ofisi ambazo haziambatani na Katiba," Gachagua alisema.

 

Madai hayo yalijiri wakati wanablogi wanaoshirikiana na vuguvugu la Tangatanga wakiripoti kwamba kulikuwa na mpango na serikali kuunda nafasi hadhi ya juu na kutajwa kama 'ofisi ya Makamu wa Rais.'

Hata hivyo, wadhifa wa makamu wa rais, ambaye alikuwa akiteuliwa na Rais, uliondolewa na Katiba ya 2010 na kubadilisha jina la ofisi hiyo hadi Naibu Rais katika katiba.

Gachagua pia alidai kuwepo mpango wa kuinyima fedha afisi ya naibu rais kupitia kupunguzwa kwa bajeti ili kudhibiti shughuli zake.

Gachagua alisema kwamba naibu rais  tayari ametengwa akidai kuwa hajaalikwa kwenye mikutano ya baraza la mawaziri na majukumu yake inasemekana yamepewa Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang'i.

"Yeye (Ruto) tayari ametengwa na amekosa kazi, kimsingi hana jukumu kabisa kwa sasa na licha ya yote hakuna wanachoweza kufanya kumfukuza kwa sababu yeye sio mteule wa mtu yeyote," alisema.

Aliendelea kusema: "Wanaweza kumnyima majukumu lakini hawawezi kumwondoa ofisini kwa sababu mpango wa awali wa kumwondoa Ruto ofisini kwa kura ya kutokuwa na imani naye ulishindwa baada ya mwasisi wake kudaiwa kuhisi kushindwa.

Kulingana na Gachagua, sehemu ya mipango ya kumfurusha Ruto  inajumuisha kumzuia asihudhurie mikutano ya baraza la mawaziri na kugawa majukumu yake kwa wadogo wake serikalini.