Mabadiliko katika usimamizi wa Amisom

Muhtasari

• Brigedia Jeff Nyagah amechukua nafasi ya Kamanda wa Sekta ya Pili ya vikosi vya KDF katika Amisom nchini Somalia.

Brigedia Jeff Nyagah akikabidhiwa uongozi wa kikosi cha sekta ya pili cha Amisom nchini Somalia.
Brigedia Jeff Nyagah akikabidhiwa uongozi wa kikosi cha sekta ya pili cha Amisom nchini Somalia.
Image: KDF

Brigedia Jeff Nyagah amechukua nafasi ya Kamanda wa Sekta ya Pili ya vikosi vya KDF katika Amisom nchini Somalia.

Alichukua wadhifa huo kutoka kwa Brigedia Paul Njema katika hafla fupi iliofanyika katika makao makuu ya Sekta ya II huko Dhobley Somalia.

Idara ya Ulinzi ilisema Brigedia Njema alikuwa kamanda wa kikosi cha tisa cha KDF kinachofanya kazi chini ya Amisom na Brig Nyagah atasimamia shughuli za kikosi cha kumi cha Amisom KDF.

Brig Njema alibainisha kuwa wanajeshi wa KDF walikuwa wamefanikiwa kudhibiti Al Shabaab katika eneo hilo na kutaka kuharibiwa zaidi kwa uwezo wao ili kuilinda Somalia na eneo hilo.

Brig Nyagah aliahidi kuendelea kufanya operesheni za kushambulia Al Shabaab ili kuleta mazingira dhabiti ya utendakazi.

"Tuna roho nzuri na tumejitolea kufikia amani na utulivu nchini Somalia kulingana na agizo la Amisom," alisema.

Aliongeza kwamba kikosi chake kitaongeza zaidi ushirikiano kati ya wanajeshi wa KDF na Vikosi vya Usalama vya Somalia kwa kufanya kazi pamoja katika operesheni zote dhidi ya Al Shabaab.

KDF ilienda Somalia mnamo Oktoba 2011. Uvamizi wa Kenya kusini mwa Somalia ulianza baada ya utekaji nyara wa wanawake wawili wa Uhispania, ambao walikuwa wakifanya kazi Katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab.

Utekaji nyara huo ulifanywa na wanamgambo wa Al Shabaab.

Operesheni Linda Nchi, miaka miwili baadaye, wanajeshi walikuwa wamefanikiwa kupata udhibiti wa  bandari ya Kismayu.