Corona: Kanisa Katoliki Tanzania limepoteza mapadri 25, watawa na wauguzi 60

Muhtasari

  • Virusi vya Corona: Kanisa Katoliki Tanzania limesema limepoteza mapadri 25, watawa na wauguzi 60 kwa matatizo ya kupumua kwa miezi 2

Katibu wa TEC Padri Charles Kitima amesisitiza tishio la corona bado lipo Tanzania
Katibu wa TEC Padri Charles Kitima amesisitiza tishio la corona bado lipo Tanzania

Baraza la Maaskofu wa Kanisa la Katoliki nchini Tanzania (TEC) limewataka wananchi wa taifa hilo la Afrika Mashariki kuchukua tahadhari zaidi dhidi ya ugonjwa wa virusi vya corona.

Katibu wa TEC Padri Charles Kitima hii leo kupitia mkutano na wanahabari amesisitiza kuwa tishio la corona bado lipo Tanzania na Kanisa na ongezeko la vifo bado linaendelea kuripotiwa ikiwemo ndani ya Kanisa lenyewe ''Ndani ya miezi iliyopita Mapadri 25 wamepoteza maisha kwa matatizo ya kupumua. Masisita na manesi zaidi ya 60. Vifo vinaendelea, tuchukue tahadhari."

Kwa mujibu wa Dkt Kitima japo serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa waraka wa kuwataka watu kuchukua tahadhari bado kuna changamoto kwa kuwa watu hawabanwi kisheria kuchukua tahadhari. ''Changamoto tuipatayo kwa kuwa serikali haijasisitiza tahadhari, watu bado wana mtazamo kuwa corona haipo au imeisha kama ilivyokuwa mwaka jana."

Dkt Kitima pia amesisitiza kutegemea sala pekee hakutaweza kuondosha tatizo hilo nchini humo. '' Mungu si hirizi, anataka binadamu tuwajibike. Corona ipo, unaambiwa chukua tahadhari unasema ushasali...Mungu wetu anataka tuwajibike , tutende majukumu yetu kwa karama na utashi tuliopewa."

Baraza la Maaskofu pia limetaka taarifa rasmi zitolewe kuhusu ugonjwa huo pamoja na kufanyika kwa tafiti juu ya ugonjwa huo na wanasayansi wa ndani.

Hii ni mara ya pili kwa mwaka huu Kanisa Katoliki nchini Tanzania kutoa tamko juu ya ugonjwa corona
Hii ni mara ya pili kwa mwaka huu Kanisa Katoliki nchini Tanzania kutoa tamko juu ya ugonjwa corona

''Ukweli huwaweka watu huru, kama mafundisho ya Biblia yanavyosema, lakini Tanzania tunaambiwa utaleta hofu. Ukweli utapatikana kwa njia ya tafiti huru."

Hii ni mara ya pili kwa mwaka huu Kanisa Katoliki nchini Tanzania kutoa tamko juu ya ugonjwa wa virusi vya corona nchini humo. Tamko la kwanza lilitolewa kwa njia ya waraka mwezi Januari ambapo Raisi wa TEC Askofu Gervaas Nyaisonga alitoa tahadhari juu ya wimbi jipya la maambukizi ya corona. Katika waraka huo kanisa lilisitiza Tanzania si kisiwa na kutaka tahadhari zote za kisayansi kuchukuliwa.

Wito wa WHO

Tahadhari hii ya Kanisa katoliki inatolewa huku Shirika la afya duniani (WHO), likiendelea pia kuitaka Tanzania kuchukua hatua zaidi kukabiliana na Covid-19.

Wiki iliyopita WHO, lilitoa wito tena wito kwa mamlaka nchini Tanzania kuanza kutoa takwimu za watu waliambukizwa ugonjwa wa Covid 19 likisema itasaidia kuwakinga Watanzania na wale wanaotangamana nao.

Katika taarifa yake ya hivi kuhusu mwenendo wa Covid 19 nchini Tanzania, shirika hilo lilielelezea wasi wasi wake kuhusu idadi ya wasafiri wa Tanzania waliopatikana na kuwa na virusi vya corona.

Shinikizo la Marekani kuhusu corona

Marekani pia imekuwa ikionesha kutoridhishwa kwake na namna Tanzania inavyoshughulikia janga la Covid-19, na mara nyingine kuonekana kuiwekea shinikizo la kutaka ichukue hatua za kisayansi kudhibiti maambukizi ya corona. Hii ni pamoja na kuwatahadharisha watu kutoizulu nchi hiyo.

Hatahivyo mwishoni mwa juma lililopita, Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulisema uko tayari kushirikiana na Tanzania kuzuia kusambaa kwa COVID-19, na kuishinda.

Katika taarifa iliyotumwa kwenye mtandao rasmi wa Ubalozi huo, Balozi wa Marekani nchini humo Dionald Wright alisema: ''Nimetiwa moyo na taarifa za hivi karibuni kutoka kwa Wizara ya Afya kukubali COVID-19 kama kipaumbele cha afya ya umma nchini Tanzania na kuwataka raia kuchukua tahadhari za kimsingi : kama vile kuepuka umati, kuvaa barakoa, na kukaa mbali. Huu ni usahuri mzuri na ninamuomba kila mmoja aufuate, anasema.

Zaidi ya kutekeleza tahadhari za dharura za kimsingi kuzuia kusambaa kwa Covid-19, Balozi Wright aliishauri Tanzania kutumia walau mbinu nyingine mbili muhimu katika kudhibiti janga la corona ya kwanza ikiwa ni kukusanya na kuripoti taarifa kuhusu upimaji na visa.

''Kwanza ili kujua kama hatua ulizochukua zinaathari ulizozilenga, ni muhimu kukusanya na kuripoti taarifa kuhusu upimaji na visa'', alisema katika taarifa hiyo.

Mbinu ya pili ni chanjo:''Kama Waziri wetu mpya wa mambo ya nje Tony Blinken alivyosema "hadi kila mtu atakapokuwa amechanjwa, hakuna yeyote ambaye ni salama kabisa."

Balozi wa Marekani nchini Tanzania ameitolea wito serikali ya Tanzania kuchukua tahadhari za kimsingi za kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya Covid -19
Balozi wa Marekani nchini Tanzania ameitolea wito serikali ya Tanzania kuchukua tahadhari za kimsingi za kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya Covid -19
Image: AFP

Akitoa mfano wa kampeni ya chanjo inayoendelea nchini mwake alisema '' Ninaitolea wito Serikali ya Tanzania kuwakusanya wataalamu wake wa afya na kutathmini ushahidi kuhusu chanjo.

Alisema Marekani kama muhisani mkubwa zaidi wa afya na msaada wa kibinadamu inaendelea kuongoza juhudi za dunia za kukabiliana na janga la Covid-19 , ikichangia zaidi ya dola bilioni 1.5 kwa ajili juhudi za kupunguza COVID-19 kote duniani na iliahidi dola bilioni 4 kwa ajili ya kuharakisha usambazaji wa chanjo.

'' Hapa nchini Tanzania, tulijitolea kutoka dola milioni 16.4 kwa ajili ya kupambana na janga la Covid-19 tangu kisa cha mtu wa kwanza kupatikana na virusi mwezi 2020. Marekani iko tayari kuongeza juhudi zetu na tuko tayari kujitolea kufanya kazi bega kwa began a Tanzania kuishinda Covid-19', amesema.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kasim Majaaliwa alitoa wito kwa watu kuchukua tahadhari dhidi ya kueneza virusi vya corona kwa kuzingatia muongozo wa afya uliyowekwa ikiwa ni pamoja na kuvalia barakoa.

Bw. Majaaliwa alisema hayo katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa katibu mkuu kiongozi Mhandisi Balozi John Kijazi aliyefariki Jumatano kutokana na ugonjwa ambao chanzo chake hakikutajwa.