Kenya kuwaweka karantini wananchi kutoka nchi sita

Muhtasari

• Ilani hiyo iliyotolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kenya -KCAA na inaanza kutekelezwa (leo) Jumatatu, Machi 8.

• Nchi zilizoathirika ni Brunei, Jamhuri ya Czech, Kuwait, Uhispania, Uswizi na Thailand.

Mlinzi ajaribu kumtuliza jamaa mmoja baada ya muda wake wa kukaa karantini kuongezwa katika chuo kikuu cha Kenyatta
Mlinzi ajaribu kumtuliza jamaa mmoja baada ya muda wake wa kukaa karantini kuongezwa katika chuo kikuu cha Kenyatta
Image: Maktaba

Serikali imetoa ilani kwa nchi ambazo wananchi wake wanapaswa kuwekwa karantini ya siku 14 kwa lazima wakati wa kuwasili Kenya.

Ilani hiyo iliyotolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kenya -KCAA na inaanza kutekelezwa Jumatatu, Machi 8.

Mkurugenzi Mkuu Gilbert Kibe wakati akithibitisha agizo hilo alisema kutengwa kwa siku 14 ni lazima kwa watu wanaotoka Brunei, Jamhuri ya Czech, Kuwait, Uhispania, Uswizi na Thailand.

"Wasafiri kutoka maeneo na nchi zilizoorodheshwa watahitajika kupitia karantini ya lazima wanapofika Kenya kwa gharama zao. Hii ni kuanzia Jumatatu tarehe 8 Machi 2021," ilisema ilani hiyo.

Ilani hiyo iliongeza kwamba wasafiri watatakiwa kuwa na cheti cha kutokuwa na virusi vya Covid-19 na vipimo kufanywa ndani ya saa 72 kabla ya kusafiri na wasionyeshe dalili zozote za homa wakati wa kuwasili.

Kibe alisema orodha ya vifaa vinavyopatikana kwa karantini vinaweza kupatikana kutoka info@kmpdc.go.ke.

Wasafiri kutoka nchi zaidi ya 200 watasamehewa kutengwa kati yao ni Tanzania.

Hii inajiri wakati Shirika la Afya Ulimwenguni na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa-CDC zimetoa tahadhari hali ya Covid-19 nchini Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu Tedros Adhanom Ghebreyesus alitaka uongozi wa Magufuli kuchukua "hatua thabiti" kupambana na hali ya Covid-19.

Tedros alisema ni jambo la kutia wasiwasi sana kwamba idadi ya watanzania wanaosafiri kwenda nchi jirani na kwingineko wamepatikana kuwa na virusi vya korona.

"Hii inasisitiza hitaji la Tanzania kuchukua hatua madhubuti, kulinda watu wao," Tedros alisema.

Kenya Jumapili iliripoti visa vipya 465 vyza Coronavirus na kufikisha idadi ya jumla ya visa  zilizothibitishwa kuwa 108,827.