Rashid Echesa kujua kama ataachiliwa ama atasalia korokoroni

Aliyekuwa waziri wa Michezo Rashid Echesa
Aliyekuwa waziri wa Michezo Rashid Echesa
Image: MERCY MUMO

Aliyekuwa waziri wa michezo Rashid Echesa anarejea mahakamani hivi leo kujua hatima yake ya dhamana.

Echesa amekuwa kizuizini tangu siku ya Ijumaa wiki iliyopita baada ya kukamatwa kwa kosa la kumshambulia afisa wa tume ya uchaguzi na mipaka (IEBC) siku ya Alhamisi.

Echesa alinaswa kwenye video akimzaba kofi afisa wa IEBC wakati wa uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Matungu katika kaunti ya Kakamega.

Kisa hiki kilitokea wakati Echesa akimshutumu afisa wa IEBC Peter Okura kwa kumzuia ajenti wa UDA kushuhudia upigaji kura.

"Sheria inasema maajenti wa uchaguzi lazima washuhudie upigaji kura!" alisikika akizungumza kwa sauti ya juu akimwuliza wakala wa IEBC.

Katika video hiyo isiosikika sana, wakala wa IEBC alijitetea akisema kwamba alikuwa akifuata maagizo.

Lakini kabla hajamaliza kuongea, Echesa alimpiga kofi.

"Uliambiwa na nani? Umeambiwa na nani? Huwezi kuweka maajenti wetu nje. Kwanini unawafukuza nje .... Huu ni upumbavu rafiki yangu ..." Echesa anasema huku akimpiga kofi afisa huyo.

Okura anadaiwa kumzuia mmoja wa mawakala wa United Democratic Alliance kuingia katika ukumbi wa kupigia kura kwa sababu hakuwa na barakoa.