Madereva Nairobi kuanza kulipia ada ya maegesho kila saa

Muhtasari

• Wenye magari katika Jiji la Nairobi wataanza kulipa ada ya maegesho ya kila saa ndani ya eneo la katikati mwa jiji.

• Malipo ya maegesho ya matatu yaliongezeka kutoka Shilingi 3,650 hadi Shilingi 5,000 kwa magari yenye viti 14 kwa mwezi.

Magari yakiwa yameegeshwa katika jiji la Nairobi
Magari yakiwa yameegeshwa katika jiji la Nairobi
Image: EZEKIEL AMING’A

Wenye magari katika Jiji la Nairobi wataanza kulipa ada ya maegesho ya kila saa ndani ya eneo la katikati mwa jiji.

Kaunti ya Nairobi inalenga kuboresha mapato yake yanayopungua ya ada ya maegesho kwa kutekeleza maegesho ya kila saa.

Waziri wa fedha katika kaunti ya Nairobi Allan Igambi alisema kaunti hiyo inaweka mikakati ya kuboresha ukusanyaji wa mapato kutoka kwa maegesho pamoja na kuongeza utekelezaji na kuboresha usimamizi wa idara hiyo.

"Ili kuongeza ukusanyaji wa mapato haswa kutokana maegesho, serikali ya kaunti itaanza kutekeleza hatua zilizotajwa kutumia teknolojia ambayo inatoa mfumo jumuishi wa elektroniki kwa majukwaa yote ya mapato na vile vile kuziba uvujaji," alisema.

Igambi pia alifichua kwamba sacco zote za magari ya uchukuzi zitapewa notisi kwa magari ambayo hayatakuwa yametimiza matakwa haya na orodha hiyo kutumwa kwa idara husika kuchukua hatua zinazohitajika.

Ada ya kuegesha ni kati ya nguzo sita muhimu za mapato kwa Kaunti ya Nairobi na zingine ni pamoja na vibali vya ujenzi na mabango na matangazo, kodi za ardhi, kibali cha biashara, kodi ya nyumba ambazo inachangia karibu asilimia 80 ya mapato ya kila mwaka ya kaunti.

Katika mwaka wa fedha uliomalizika Juni 30, 2020, ada ya maegesho ilichangia jumla ya shilingi bilioni 1.54 dhidi ya lengo la bilioni 2.76. Shilingi bilioni 1.9 zilikusanywa dhidi ya lengo la bilioni 3 mwaka 2018-19 huku bilioni 1.9 zilikusanywa mwaka 2017-18.

Mwezi Septemba mwaka jana, bunge la kaunti lilipitisha Muswada wa Fedha wa Kaunti ya Nairobi, 2019, likiruhusu  kaunti kutoza ada ya maegesho ya Shilingi 400 kila siku katika eneo la CBD kuanzia Desemba 4.

Malipo ya maegesho yaligawanywa kama Kanda ya Kwanza (CBD) kwa Shilingi 400, Kanda ya Pili (Parklands, Westlands na Upper Hill) Shilingi 300, Kanda ya Tatu (vituo vya kibiashara) Shilingi 200.

Viwango vya maegesho ya barabarani kila siku kwa malori viliwekwa shilingi 1,000 na trela shilingi 3,000.

Malipo ya maegesho ya matatu yaliongezeka kutoka Shilingi 3,650 hadi Shilingi 5,000 kwa magari yenye viti 14 kwa mwezi.

Matatu za viti thelathini na mbili zitalipa Shilingi 8,000 kutoka 5,200 wakati mabasi yenye viti 51 yakitozwa shilingi elfu kumi kutoka 7,500.  

Mnamo Desemba mwaka jana, wenye magari ya uchukuzi wa umma Nairobi walikataa kuongezwa kwa ada ya maegesho.

Shirikisho la Wenye magari lilishtaki kuzuia kuongezeka kwa ada ya maegesho.

Korti iliamuru kaunti kubadilisha ada ya maegesho kutoka Shilingi 400 hadi 200.

Wiki iliyopita, Jaji Anthony Mrima alitoa agizo la kuongezwa kwa ada hiyo hadi Aprili 21.