Millicent Omanga azua vurugu ofisini NCIC kwa madai kwamba wakati wake umeharibiwa

Muhtasari
  • Millicent Omanga azua vurugu ofisini NCIC, huku akisema wakati wake umeharibiwa na tume hiyo
  • Pia alitaka kujua kwanini waliitwa wote wakati siku moja
Millicent Omanga
Image: Andrew Kasuku

Seneta Mteule wa chama cha Jubilee Millicent Omanga Jumatatu, Machi 8 alizua  vurugu katika afisi za Tume ya Uwiano na Utangamano wa kitaifa, NCIC.

Kupitia kwenye video iliyoenea sana kwenye mitandao ya kijamii Milicent alisikika akilalamika kwanini NCIC iliamua kuita wanasiasa waliotakiwa kuenda mbele ya tume hiyo wakati mmoja.

Omanga alikuwa amefika katika afisi hizo kujibu madai ya uchochezi katika chaguzi ndogo zilizofanyika katika eneo bunge la Matungu na Kabuchai wiki jana.

Akiwa mwingi wa hasira, Omanga aliwakashifu maafisa wa tume ya NCIC kwa kuchukua muda wake mwingi ikizingatiwa alikuwa ahojiwa saa tano asubuhi lakini kufikia saa sita mchana hakuwa amehojiwa.

Wakati alipozua kizaazaa hicho, mbunge mwenzake wa Kasipul Charlse Were ndiye alikuwa bado anahojiwa na maafisa hao.

Kulingana na Omanga, tume hiyo ilimtaka afike afisini humo mwendo wa saa tano asubuhi lakini alighadhabishwa baada kusubiri kwa muda wa zaidi ya saa moja kuhojiwa.