Marekani: mapendekezo kwa waliochanjwa kukutana bila barakoa

Muhtasari

• Zaidi ya Wamarekani milioni 30 tayari wamepatiwa chanjo hiyo kufikia sasa.

• Wamarekani waliochanjwa na kumaliza dozi yao, wanaweza kukutana ndani ya chumba na watu wengine waliopewa chanjo bila kuvalia barakoa ama kukaa mbalimbali.

Watu wakipatiwa chanjo ya corona Marekani
Watu wakipatiwa chanjo ya corona Marekani
Image: GETTY IMAGES

Kituo cha afya na magonjwa nchini Marekani CDC kimetangaza kwamba Wamarekani waliopatiwa chanjo ya corona wanaweza kurudia katika hali yao ya kawaida.

Wale ambao wamepokea chanjo zinazohitajika wanaweza kutembeleana na watu wengine waliopatiwa chanjo na baadhi ya watu ambao hawajapata chanjo kulingana na masharti hayo mapya.

''Watu huwa wamelindwa wiki mbili baada ya kupewa dozi ya mwisho ya chanjo yao'', kituo hicho kilisema.

Zaidi ya Wamarekani milioni 30 tayari wamepatiwa chanjo hiyo kufikia sasa.

Maafisa wa Afya walitangaza maelezo hayo mapya ya afya wakati wa kikao cha jopo la virusi vya corona siku ya Jumatatu kilichofanyika katika Ikulu ya Whitehouse.

Mapendekezo hayo yanasema kwamba Wamarekani waliochanjwa na kumaliza dozi yao, wanaweza kukutana ndani ya chumba na watu wengine waliopewa chanjo hiyo bila kuvalia barakoa ama kukaa mbalimbali.

Wanaweza kukutana ndani ya chumba na watu ambao hawajapewa chanjo kutoka nyumba moja , iwapo hawapo katika hatari ya kuugua na virusi hivyo.

Wanaweza kutopimwa ama kutojitenga wanapokutana na watu walioambukizwa, hadi pale dalili zitakapojitokeza.

''Tumeanza kuelezea jinsi ulimwengu utakavyokuwa tunapoanza maisha bila Covid-19'', afisa mwandamizi Andy Slavitt aliambia maripota.

''Huku watu zaidi wakiendelea kupatiwa chanjo....orodha ya hatua kama hizo zitaendelea kuchukuliwa''.

Wale watakaochanjwa watahitajika kufuata kanuni nyengine za kujilinda , kama vile kuvalia barakoa na kukaa mbali katika maeneo ya umma mbali na kujiepusha na makundi makubwa na kusafiri.

Maelezo hayo pia yanatoa wito wa kuvalia barakoa na kukaa mbali na wale ambao hawajapokea chanjo na ambao wapo katika hatari ya shida zinazohusiana na virusi vya corona.

Marekani imeshuhudia ongezeko la idadi ya watu wanaopatiwa chanjo kwa siku. Zaidi ya chanjo milioni 90 zimetolewa kufikia sasa.

Kuidhinishwa kwa chanjo ya tatu Johnson and Johnson pia kumeimarisha usambazaji wa chanjo.

Lakini maafisa wa afya walionya kwamba Covid-19 bado ni ugonjwa unaotia wasiwasi.

''Zaidi ya asilimia 90 ya idadi ya watu bado haijapata chanjo'' , Mkurugenzi wa CDC Dkt Rochelle Walenskey alisema.

Jukumu letu ni kuhakikisha kwamba iwapo kuna visa vipya 60,000 tunawalinda walio hatarini kuambukizwa.

Marekani imeripoti zaidi ya maambukizi milioni 29 na vifo 525,000.

Dkt. Walensky aliongezea kwamba mwongozo utaendelea kuimarishwa huku watu zaidi wakiendelea kupata chanjo mbali na sayansi na ushahidi ukiimarika.

Bwana Slavitt alisema kwamba ni alfajiri ilio na matumaini lakini ikizingatia maonyo katika siku za usoni.

Wiki iliopita bwana Biden alisema kwamba Marekani itakuwa na chanjo za kutosha kwa kila mtu mzima mwisho wa mwezi Mei.