Jamaa aliyemdhulumu mshukiwa Mombasa afikishwa mahakamani

Muhtasari

• Swabir Abdulrazaq Mohamed alikamatwa siku ya Jumatatu na maafisa wa upelelezi baada ya video yake kuenea mitandaoni.

Swabir Abdulrazaq Mohamed
Swabir Abdulrazaq Mohamed
Image: DCI

Mwanamume aliyenaswa kwenye video akimdhulumu mshukiwa wa wizi mjini Mombasa anatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi leo.

Swabir Abdulrazaq Mohamed alikamatwa siku ya Jumatatu na maafisa wa upelelezi baada ya video yake kuenea mitandaoni.

Atafikishwa mahakamani kukabiliwa na mashtaka ya kumdhulumu na kumsababishia mwenzake majeraha na huenda pia akakabiliwa na shtaka lingine la kujaribu kuua.

Swabir mwenye umri wa miaka 33 ni msimamizi wa walinzi katika kampuni moja eneo la Shimanzi Mombasa na inasemekana jamaa aliyekuwa akidhulumiwa huenda alikuwa ameiba au kuingia ndani ya kampuni hiyo bila idhini.

Katika video hiyo iliyoibua hisia kali mtandaoni Swabir anaonekana akimfanyia madhila mshukiwa kwa kuasha moto kwenye neti ya plastiki na kuishikilia juu ya mshukiwa aliyekuwa akiangukiwa na matone ya moto.

Anasikisha akilia kwa uchungu huku mikono yake ikiwa imefungwa kwa Kamba na kulazwa juu ya gurudumu la gari.  

Maafisa wa polisi hata hivyo bado hawajafanikiwa kumpata jamaa aliyekuwa akidhulumiwa. Wamepuuzilia mbali madai ya Swabir kwamba alimkabidhi jamaa huyo kwa polisi kwa sababu hata hakumbuki kituo kipi alimpeleka.