KQ yasitisha safari za kwenda Uingereza kuanzia Aprili 9

Muhtasari

• Shirika hilo lilisema wale ambao wataamua kufutilia mbali safari zao watarejeshewa pesa zao zote bila penalti yoyote.

• Serikali ya Kenya ilipiga marufuku safari zote za ndege kutoka uingereza kuingia nchini Kenya kuanzia saa sita usiku wa Aprili 9.

Shirika la ndege nchini, Kenya Airways (KQ) limetangaza kusitisha safari za kwenda nchini Uingereza.

KQ katika taarifa yake siku ya Jumatatu Aprili 5, 2021 ilisema kwamba itasitisha safari zake kuanzia Aprili 9, 2021 kuambatana na agizo la serikali ya Kenya kuhusu abiria kutoka Uingereza.

Serikali ya Kenya ilipiga marufuku safari zote za ndege kutoka uingereza kuingia nchini Kenya kuanzia saa sita usiku wa Aprili 9.

Kutokana na agizo la serikali ya Kenya na kufuatia kuongezeka kwa idadi ya wasafiri wanaotaka kusafiri kabla ya siku ya makataa kampuni ya Kenya Airways Q imesema kwamba itaongeza ndege mbili zaidi katika safari za kwenda Uingereza tarehe 7 na 8.

Kulingana na taarifa ya shirika hilo wasafiri wote waliokuwa tayari wamekata tikiti za kusafari kuanzia tarehe 9, wameshauriwa kubadili safari zao na kusafiri kabla ya tarehe hiyo au kufutilia mbali safari zao.

Shirika hilo lilisema wale ambao wataamua kufutilia mbali safari zao watarejeshewa pesa zao zote bila penalti yoyote.

Wateja wana hadi Machi 31, kutumia tiketi zao.