Habari za sasa! Atwoli achaguliwa tena kuongoza COTU

Muhtasari

• Atwoli alichaguliwa bila kupingwa siku ya Ijumaa na sasa atahudumu kwa kipindi kijacho cha miaka mitano tena.

• Katibu mkuu wa muungano wa wauguzi nchini Seth Panyako alikuwa ameonyesha ari ya kutaka wadhifa huo.

 

Katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli
Katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli
Image: MAKTABA

Katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli amechaguliwa tena kuongoza muungano huo kwa muhula wa tano wa miaka mitano.

Atwoli alichaguliwa bila kupingwa siku ya Ijumaa na sasa atahudumu kwa kipindi kijacho cha miaka mitano tena.

Kupitia akaunti yake ya Twitter siku ya Ijumaa, Atwoli aliwapongeza wafanyikazi nchini kwa kuendelea kuwa na imani katika uongozi wake.

 

"Naahidi kuwatumikia kwa nguvu zangu zote na kutosaliti imani mliyonipa," alisema.

Katibu mkuu wa muungano wa wauguzi nchini Seth Panyako alikuwa ameonyesha ari ya kutaka wadhifa huo.

Katibu mkuu wa muungano wa kitaifa wa Wauguzi - KNUN Seth Panyako
Seth Panyako kutoka muungano Wauguzi Katibu mkuu wa muungano wa kitaifa wa Wauguzi - KNUN Seth Panyako

Panyako na miungano kadhaa ya wafanyikazi walikuwa wamemshutumu Atwoli kwa kutumia mbinu mbovu kuwaondoa wapinzani wake kwenye kinyang’anyiro hicho ili iwe rahisi kwake kurejea ofisini.

Miungano mingine iliyokuwa inaunga mkono kauli ya Panyako ni : Chama cha Kitaifa cha Wafanyikazi wa Nyumbani, Chama cha Wafanyikazi wa Ubunifu wa Kauri, Chama cha Wafanyikazi wa Uchukuzi wa Umma, Chama cha Wafanyikazi wa Bonde la Ufa na Umoja wa Wafanyikazi wa Sekondari Wasiofundisha.

Atwoli amehudumu katika wadhifa huo tangu 2001 baada ya kutwaa mamlaka kutoka kwa marehemu Joseph Mugalla.