ODM yakataa kujiondoa kutoka uchaguzi wa Bonchari kuunga mkono Jubilee

Muhtasari

• Msururu wa mikutano ikiwa ni pamoja na mkutano uliyoongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang'i siku ya Jumatano, haikufaulu kupata mwafaka kuhusu unchaguzi huo wa Mei 19.

TAARIFA YA JAMES MBAKA 

Raila Odinga amekataa shinikizo za wandani wa Rais Uhuru Kenyatta kumwondoa mgombea wa ODM katika uchaguzi mdogo wa Bonchari na kuunga mkono muaniaji wa Jubilee.

Msururu wa mikutano ikiwa ni pamoja na mkutano uliyoongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang'i siku ya Jumatano, haikufaulu kupata mwafaka kuhusu unchaguzi huo wa Mei 19.

Vyama vya Jubilee na ODM vina makubaliano ya kufanya kazi pamoja na na vimeshirikiana katika chaguzi ndogo zilizopita lakini katika eneo bunge la Bonchari kila chama kimewasilisha mgombeaji.

Kufuatia mkutano huo katika ofisi ya Matiang'i Harambee House, Raila aliwaita wandani wake pamoja na viongozi kutoka Kisii nyumbani kwake mtaani Karen. Huko, alitangaza kwamba ODM haitaondoa mgombeaji wake.

Waziri wa Usalama wa ndani Fred Matiang'i

Uamuzi huo wa Raila ulionekana kama mikakati ya kisiasa ya ODM kuimarisha ubabe wake katika eneo la Kisii kuzuia chama cha UDA cha Naibu Rais William Ruto kupenya ngome hiyo.

“Tuko Bonchari kushinda uchaguzi mdogo. Nataka kuona ushindi katika Bonchari. Nina habari yangu mwenyewe kwamba mgombea wetu ndiye mwenye nguvu zaidi. Wacha tuendelee, ”Raila aliwaambia wandani wake mtaani Karen.

Meza yetu ya habari iligundua kuwa mkutano huo wa Karen usiku ulikuwa kilele cha juhudi za viongozi wa Jubilee na ODM kutafuta mwafaka.

Mkutano wa Harambee ulihudhuriwa na miongoni mwa wengine Matiang'i, Gavana wa Kisii James Ongwae, Seneta Sam Ongeri, katibu mkuu wa Jubilee Raphael Tuju, kaka wa Raila Oburu Odinga na Mweka Hazina wa ODM Timothy Bosire.

Katibu mwandamizi wa Mambo ya Ndani na Uratibu wa Serikali ya Kitaifa Winnie Guchu pia alihudhuria mkutano huo uliochukuwa saa mbili.

Ikiwa makubaliano yangefaulu, ODM ingemwondoa Parvel Oimeke ili kumuunga mkono Zebedeo Opore wa Jubilee.