Tutarajie nini katika hotuba ya Rais Samia bungeni hii leo?

Muhtasari

• Rais Samia Suluhu Hassan leo anatarajiwa kuhutubia Bunge la Tanzania katika hotuba itakayotoa mwelekeo wa nini hasa amepanga kutimiza katika muhula wake wa kwanza madarakani.

Image: IKULU TANZANIA

Rais Samia Suluhu Hassan leo anatarajiwa kuhutubia Bunge la Tanzania katika hotuba itakayotoa mwelekeo wa nini hasa amepanga kutimiza katika muhula wake wa kwanza madarakani.

Hii itakuwa ni mara yake ya kwanza kufanya hivyo tangu aapishwe kuwa Rais Machi 19 mwaka huu, baada ya kifo cha cha ghafla cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati Rais John Magufuli kilichotokea Machi 17 mwaka huu.

Swali kubwa ambalo watu wengi wanajiuliza ni nini hasa Rais Samia atawaambia Watanzania na dunia nzima kwa ujumla leo katika hotuba yake hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa?

Ni majipu, tabasamu au macho?

Hotuba ya Rais kwa Bunge umekuwa ni utaratibu wa kawaida wa Tanzania ambapo Rais - ambaye kikatiba ni sehemu ya Bunge, hupata fursa ya kuzungumza na wananchi kupitia chombo na kutoa mwelekeo wa nini hasa serikali yake imepanga kufanya katika kipindi cha miaka mitano ya muhula wake.

Katika historia ya Tanzania, Samia ni Rais wa kwanza ambaye atalazimika kutoa mwelekeo wake katika kipindi cha miaka minne ijayo; kwa sababu hakupatikana kutokana na Uchaguzi Mkuu kama walivyokuwa watangulizi wake bali kutokana na mazingira ya kifo cha mtangulizi wake.

Utawala wake unajulikana kama Utawala wa Awamu ya Sita kwa sababu ingawa alikuwa na Magufuli kwenye Awamu ya Tano, halazimiki kufuata kila kilichokuwa kinafuatwa na mtangulizi wake huyo- hata kama waliomba tiketi kwa pamoja wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2020.

Image: BUNGE

Kwa kawaida, hotuba za namna hii huenda sambamba na tukio la kufunga au kufungua Bunge, na kwa sababu kazi ya kuzindua Bunge la 12 ilishafanywa na Magufuli takribani miezi mitano iliyopita, kazi ya Samia itakuwa ni kutoa tu maelezo yake kuhusu mwelekeo wa utawala wake pekee.

Kihistoria, hotuba za kuhutubia Bunge huwa ni ndefu na hugusa karibu maeneo yote muhimu ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Kwa sababu ya urefu huo, Watanzania hukumbuka hotuba za viongozi wao katika siku hiyo kutokana na mambo ambayo si ya kisera zaidi bali kutokana na mwonekano au namna watu walivyokuwa wakimfahamu kabla.

Kwa mfano, katika hotuba yake ya kufungua Bunge baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Rais Jakaya Kikwete, aliwaambiwa Watanzania kwamba ingawa sura yake ni ya bashasha na kuonekana kama anabasamu muda wote, yeye si mtu wa kuchekea mambo yasiyo na maana na kwamba kwenye mazito, yeye ni mtu makini na tabasamu lake lisiwadanganye watu.

Ilipofika zamu ya Magufuli mwaka 2015, yeye aliwaambia Watanzania kwamba serikali yake itakuwa ni ya "kutumbua majipu"- akitumia sehemu kubwa ya hotuba yake kueleza namna ambavyo hatavumilia utendaji kazi usioridhisha na ufisadi katika wakati wake madarakani.

Wiki chache zilizopita, wakati wa tukio la Rais Samia kuapisha baadhi ya makatibu wakuu wa wizara na watendaji wakuu wa taasisi za umma, alieleza kwamba ingawa macho yake yanaonekana yamelegea, yanaona vizuri.

Vyovyote itakavyokuwa, itakuwa vigumu kwa Watanzania kukumbuka kila atakachozungumza katika hotuba yake hiyo lakini kuna mstari au sentesi moja ambayo itabaki katika kumbukumbu zao kwa muda mrefu.

Mambo yanayotajwa kuweza kuzungumzwa

Rais Samia ameingia madarakani katika wakati ambao kuna mgawanyiko wa wazi kuhusu nini hasa ni urathi (legacy) wa mtangulizi wake. Wanaompenda hayati Magufuli, wanampenda kwa moyo wao wote na wale wanaomchukia, inaonekana wanamchukia kwa moyo wao wote pia.

Kwa wafuasi wa Magufuli, urais wake utakumbukwa kwa ujenzi wa miundombinu kama vile barabara, madaraja, ununuzi wa vivuko na ndege za serikali. Magufuli pia alipunguza mivutano ya mara kwa mara kati ya serikali na wafanyabiashara wadogo (Wamachinga), kutovumilia uzembe, kutosafiri kwenda ughaibuni na hivyo kuokoa matumizi ya fedha, kuboresha huduma za serikali na masuala mengine ya kiutendaji.

Image: BUNGE

Wakosoaji wake wanamweleza kama mtu aliyeongoza kwa mkono wa chuma - akibinya uhuru wa vyombo vya habari, akibana vyama vya siasa na asasi za kiraia, akionekana kupendelea vyombo vya serikali na vya umma kwenye biashara badala ya sekta ya binafsi huku utawala wake ukigubikwa na madai ya kubambikia watu kesi - na kuwaweka ndani pasipo makosa ya wazi.

Katika usuli huo, Rais Samia anatarajiwa kutoa hotuba itakayokuwa na misukumo mikubwa miwili - mosi kujaribu kuwapoza wale ambao waliumizwa na utawala wa mtangulizi wake na pili kutowanyong'onyeza wale waliokuwa wakimuunga mkono Magufuli.

Hii maana yake ni kwamba, hotuba yake italazimika kuwa na maelezo ya kuendeleza pale alipoishia Magufuli - kwa kumalizia miradi mikubwa ya ujenzi aliyoiacha, kupambana na ufisadi, kutetea wanyonge na kuhakikisha huduma za afya na elimu zinaendelea kuwafikia wananchi wengi zaidi wa hali ya chini.

Wakati huohuo, hotuba yake pia inaweza kuzungumzia masuala kama ya kuachia vyombo vya habari na asasi za kiraia uhuru wa kufanya shughuli zao, kutoa msimamo wa kuzimua sekta binafsi, kupinga uonevu na kubambikia watu kesi huku akitaka viongozi wake kuwa mfano kwa kufuata na kutii sheria za nchi.

Katika mwezi wake wa kwanza madarakani, Rais Samia ameonyesha kwamba hatafuata baadhi ya misimamo yenye utata ya utawala wa Magufuli, lakini pia hatakwenda mbali sana na mtangulizi wake huyo.

Katika hotuba yake aliyoitoa Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita katika mkutano na viongozi wa dini, Samia alisisitiza kwamba yeye na Magufuli ni kama timu moja na hivyo hakuna sababu ya watu kuanza kuwapima na kuwatofautisha kiutawala.

Hata hivyo, Samia pia amezungumza hadharani kuhusu namna asivyofurahishwa na vitendo vya wananchi kubambikiwa kesi, kuwekwa magerezani pasipo kukamilika kwa uchunguzi na vikwazo dhidi ya wawekezaji - mambo ambayo yanahusishwa moja kwa moja na utawala wa Rais wa Tano wa Tanzania.

Ni bahati mbaya au bahati kwa Samia?

Tayari, baadhi ya viongozi wa upinzani wameanza kutoa maoni na matarajio yao kuhusu nini hasa wanakitarajia kutoka kwenye hotuba ya Rais Samia - wengi wakisisitiza kwamba hotuba hiyo ni lazima ibebe matumaini ya Watanzania kwa serikali yao.

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ameandika katika mtandao wa twitter Aprili 21, mwaka huu na kusema kwamba anatarajia hotuba ya Samia itatotoa kipaumbele katika ulinzi wa Utawala wa Sheria na Katiba ya Tanzania.

" Ni matarajio yangu kwamba Katiba itaheshimika, sheria ya vyama vya siasa itaheshimika ili vyama viweze kufanya shughuli zake bila bughudha wala kusukwasukwa na vyombo vya dola. Wanasiasa watakuwa huru kukosoa bila kukamatwa na tutarudi kwenye siasa za ushawishi," aliandika Zitto.

Samia, katika sadfa ya kipekee, anakuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kuzungumza bungeni kwa mara ya kwanza akiwa amepata fursa ya kuzungumza na wateule wake wengine na kusoma katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuhusu nini kinazungumzwa baada ya yeye kutoa kauli.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Hii ni bahati ambayo watangulizi wake hawakuwa nayo. Mara nyingi watangulizi wake walikuwa wakienda bungeni siku chache tu baada ya kumalizikika kwa uchaguzi na mijadala ikiwa inatawala bado kuhusu uhalali wa uchaguzi na akina nani wameshinda au kushindwa katika uchaguzi.

Samia atazungumza wakati watu wakiwa tayari wameanza kutoa mwelekeo wa nini wanataraji kutoka kwake - mijadala inayoendelea bungeni ikiwa ni ushahidi wa taifa lililogawanyika kuhusu nini hasa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatarajiwa kuendelea nacho katika miaka minne ya Samia.

Jambo pekee lililo wazi ni moja; kwamba Samia atataka kutoa hotuba ambayo kama atatimiza aliyoahidi kwa kiasi kikubwa, atakuwa amekaribia lengo lake muhimu la kisiasa - kukisaidia chama chake kushinda katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025.

Rais Samia atakuwa na kazi kubwa mbili leo - kuunganisha taifa kupitia hotuba yake hiyo na kurejesha kuaminika tena kwa CCM kama mtetezi wa demokrasia si Tanzania pekee, lakini katika eneo zima la Afrika Mashariki.