Serikali yaondoa hofu kuhusu uhaba wa ARVs

Muhtasari

• Waziri wa Afya Mutahi Kagwe siku ya Jumatatu aliwahakikishia wakenya kuwa kwa sasa wana dawa za kutosha hadi mwezi Agosti na kwamba tayari wameagiza dawa zingine. 

 Serikali imeondoa hofu kuhusu uhaba wa dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi nchini ARV’s.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe siku ya Jumatatu aliwahakikishia wakenya kuwa kwa sasa wana dawa za kutosha hadi mwezi Agosti na kwamba tayari wameagiza dawa zingine. 

Kagwe alisema kwamba vuta ni kuvute iliyokuwepo baina ya serikali la shirika la USAID na ambayo ilikuwa imesababisha kuzuiliwa kwa shehena ya dawa za ARV bandarini imetatuliwa. 

Alisema serikali kupitia wizara ya fedha ililipa ushuru uliyohitajika kabla ya dawa hizo kuachiliwa.

Baadhi ya wabunge wengi wao kutoka maeneo ya Nyanza walikuwa wametoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati mzozo kati ya serikali na shirika la USAID ambao ulikuwa umezuia kutolewa kwa ARVs na bidhaa zingine muhimu za kukabiliana na virusi vya ukimwi nchini.

Viongozi hao walionya kuwa vituo vya afya katika maneo mengi vilikuwa tayari vinakabiliwa na uhaba wa dawa muhimu. Hali iliyokuwa inahataraisha maisha ya maelfu ya watu.

“Tunajali watu wetu. Tuna wasiwasi kuwa tutapata vifo vingi, labda zaidi kuliko vile vya Covid-19, ,"mwakilishi wa wanawake wa Homa Bay Gladys Wanga alisema.

Shirika la USAID, ambalo ni mdhamini mkuu wa dawa hizo, limebadili mfumo wake wa usambazaji wa dawa hizo kupitia shirika la Kemsa na kuamua kuleta dawa hizo kupitia shirika la kibinafsi la Kimarekani Chemonics International.

Kutokana na hatua hiyo shehena ya takriban shilingi bilioni 1.1 imekuwa ikilala bandarini tangu Januari 18 kutokana na ushuru wa takriban shilingi  milioni 90.

Baada ya kuachiliwa kwa shehena hiyo sasa malumbano mengine yameibuka kuhusu nani anafaa kusambaza dawa hizo huku USAID ikisisitiza kwamba ni shirika la Chromonics litasambaza nayo serikali ikishikilia kwamba ni shirika kemsa lenye jukumu la kusambaza dawa hizo.