Serikali yataka maafisa 6 walioshtakiwa kwa mauaji ya ndugu wawili Kianjokoma wasiachiliwe kwa dhamana

Muhtasari

•Kupitia wasilisho ambalo lilitolewa mahakamani  na IPOA, serikali inataka maafisa hao wazuiliwe hadi wakati kesi dhidi yao itasikizwa na kuamuriwa.

•Shuhu amesema kuwa maafisa hao bado wako na madaraka ya polisi ikiwemo kutumia bunduki, kukamata na kuzuilia watu na huenda wakarejelea kazi zao iwapo wataachiliwa huru.

Image: Maktaba

Habari na Annette Wambulwa

Serikali imepinga kuachiliwa kwa dhamana kwa maafisa sita walioshtakiwa kwa mauaji ya ndugu wawili kutoka Kianjokoma mwezi uliopita.

Kupitia wasilisho ambalo lilitolewa mahakamani  na IPOA, serikali inataka maafisa hao wazuiliwe hadi wakati kesi dhidi yao itasikizwa na kuamuriwa.

Afisa mpelelezi mwandamizi Ibrahim Shuhu amesema kwamba sita hao hawajahitimu kuachiliwa kwa dhamana kwani upande wa mashtaka uko na ushahidi mkubwa unaoashiria kuwa wako na hatia.

Shuhu amesema kuwa maafisa hao bado wako na madaraka ya polisi ikiwemo kutumia bunduki, kukamata na kuzuilia watu na huenda wakarejelea kazi zao iwapo wataachiliwa huru.

Mpelelezi huyo amesema kuwa huenda washukiwa wakaharibu ushahidi kuona kwamba tayari kulikuwa na jaribio la kuficha ukweli kuhusu yaliyotokea  kwa kusema kuwa ilikuwa ajali ilhali kuna mashahidi ambao walisema waliona na kusikia ndugu wale wawili wakishambuliwa.

Shuhu amedai kwamba hatua ya kuachiliwa kwa washukiwa hao itakuwa ya dhuluma kwa familia ya marehemu/.

Jaji Daniel Ogembo anatarajiwa kusikiza kesi ya dhamana iliyowasilishwa na washukiwa siku ya leo (Jumatani) kabla ya kufanya uamuzi wake.