Ruto amtaka Raila kuacha kutumia fujo kwa kampeini

Muhtasari

• Ruto alimtaka Raila kujitolea kwa Wakenya kwamba ataheshimu uamuzi wa wapiga kura wa Kenya katika uchaguzi wa Agosti.

• Alimtahadharisha Bw Odinga dhidi ya kuendeleza "siasa za ngome" ambazo zinatishia umoja wa nchi, akitaja ghasia alizodai kufadhiliwa na ODM huko Kondele na Embakasi Mashariki.

Naibu rais William Ruto akifanya kampeini
Naibu rais William Ruto akifanya kampeini

Naibu Rais William Ruto amemtaka kinara wa Upinzani Raila Odinga kukoma kutumia ghasia kupata urais.

Ruto alimtaka Bw Odinga akome kuhalalisha ghasia, awajibike na kuweka mikakati ya kukabiliana na maovu ndani ya chama chake kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Akizungumza siku ya Alhamisi Naibu Rais alimwambia Waziri Mkuu huyo wa zamani kuhakikisha ODM inaendesha kampeni za amani na kudumisha amani wakati na baada ya uchaguzi.

“Ninataka kuuliza ODM na kinara wake Raila Odinga kuacha ghasia. Hawezi kuendelea kutoa visingizio kuhusu ghasia,” akasema Ruto.

Akizungumza katika Kaunti ya Machakos, Ruto alisema utumiaji wa ghasia na Odinga kuwatisha wapinzani wake  ni jambo ambalo limepitwa na wakati.

Alisema hulka ya kuwarushia mawe washindani wake haitamletea kura.

Alimtahadharisha Bw Odinga dhidi ya kuendeleza "siasa za ngome" ambazo zinatishia umoja wa nchi, akitaja ghasia alizodai kufadhiliwa na ODM huko Kondele na Embakasi Mashariki.

Ruto alimtaka Raila kujitolea kwa Wakenya kwamba ataheshimu uamuzi wa wapiga kura wa Kenya katika uchaguzi wa Agosti.

"Lazima wajitolee kwamba watakubali uamuzi wa watu wa Kenya na kwamba hawatajiapisha, kuandaa maandamano au kusababisha vurugu," alisema Naibu rais.

Naibu Rais alisema hakuna haja ya viongozi kuwatumia vijana kusababisha vurugu, akisema badala yake wanapaswa kubuni mpango wa kuwatengenezea nafasi za kazi.

"Iwapo ningewashauri washindani wangu, ningewaambia wabuni ajenda nyingine kwa vijana kwa sababu vurugu hazitawapa kura," alisema Ruto.

Maoni yake yaliungwa mkono na baadhi ya wabunge wa mrengo wa Hustler Movement waliotaka kampeni za amani zifanyike bila vurugu, ukabila na siasa za migawanyiko.

Walikuwa wabunge Victor Munyaka (Machakos town,) Vincent Musyoka (Mwala), Nimrod Mbai (Kitui Mashariki), Ndindi Nyoro (Kiharu), John Mwirigi (Igembe Kusini) na aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnston Muthama.