Museveni na Kagame waafikia kumaliza mgogoro baina ya Uganda na Rwanda

Muhtasari

•Wamesaini makubaliano ya amani katika mji mkuu wa Angola, Luanda kumaliza uhasama uliopo kati ya mataifa hayo jirani

•Walifikia makubaliano hayo katika mkutano wa pili huko Luanda mbele ya marais wa Jamhuri ya Kidmeokrasi ya Congo , Angola na rais wa Congo Brazaville waliokuwa wapatanishi katika mgogoro huo

IKULU RWANDA
IKULU RWANDA

Marais Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda wametia saini makubaliano ya amani katika mji mkuu wa Angola, Luanda kumaliza uhasama uliopo baina ya mataifa hayo jirani.

Waliafikia makubaliano hayo katika mkutano wa pili mjini Luanda mbele ya marais wa Jamhuri ya Kidmeokrasi ya Congo , Angola na Congo Brazaville waliokuwa wapatanishi katika mgogoro huo.

Joto la kisiasa limekuwepo tangu mwanzoni mwa mwaka huu na limeathiri maisha ya watu kijamii na kiuchumi katika mataifa hayo jirani.

Maafisa nchini Rwanda wameishutumu Uganda kwa kuwafunga na kuwatesa kinyume cha sheria raia wake nchini Uganda, wakati Uganda nayo ikiishutumu Rwanda kwa kutekeleza ujasusi katika ardhi yake.

"Tutashughulikia matatizo haya yote", rais Kagame amewaambia wandishi habari baada ya kusaini makubaliano hayo.

Makubaliano ya leo yamefikiwa baada ya "jitihada zilizoidhinishwa na Angola kwa usaidizi wa DR Congo" kwa mujibu wa ikulu ya Angola.

Viongozi hao wawili wamekubaliana kutilia mkazo kutatua mzozo wowote baina ya mataifa yao kwa njia amani shirika la habari nchini Angola, Angop linaripoti.

Mnamo machi mwaka huu katika hotuba kwenye mkutano wa kitaifa, Rais wa Rwanda Paul Kagame ameelezea kuwa chimbuko la mgogoro baina ya nchi yake na nchi ya Uganda ni la tangu miaka 20 iliyopita nchi ya Uganda ikitaka kuangusha utawala wake.

Rais Kagame amesema mgogoro huo ulishika kasi hivi karibuni kufuatia wananchi wa Rwanda wanaoingia nchini Uganda au kufanyia kazi nchini humo kushikwa na kuzuiliwa sehemu ambazo hazijulikani na kufanyiwa vitendo vya mateso huku akishtumu utawala wa Uganda kutoa nafasi ya ushirikiano kwa kundi la Rwanda National Congress linaloongozwa na mkuu wa zamani wa majeshi ya Rwanda jenerali Kayumba Nyamwasa:

''RNC wanafanya kazi kwa ushirikiano na vyombo vya usalama vya Uganda.kilicho wazi ni kwamba Wanachokifanya ni kunyanyasa wanyarwanda ambao hawataki kuungana nao huku wakiwasingizia a kwamba wametumwa na utawala wa Kigali kuhujumu usalama wa Uganda na kuuwa wanyarwanda wa upinzani.Ni madai yasiyo na msingi.lakini haya yote yanaonyesha ushirikiano wa dhati uliyopo baina ya serikali ya Uganda na kundi la RNC