Viongozi wa Murang'a wampa Raila Odinga viatu 'waterproof' vya kumsaidia kukwea Mlima

Muhtasari

•Raila aliwaomba Wakenya kuwa na matumaini huku akiahidi kwamba mambo mazuri yaja hivi karibuni.

•Baada ya kinara wa ODM kupokea zawadi hiyo wahubiri waliokuwa wamehudhuria hafla hiyo walipiga  dua wakimtakia neema anapofanya kampeni zake katika eneo hilo.

Raila Odinga akabidhiwa viatu vya kukwea Mlima na viongozi wa Murang'a
Raila Odinga akabidhiwa viatu vya kukwea Mlima na viongozi wa Murang'a
Image: SABINA CHEGE FOUNDATION

Siku ya Jumamosi kinara wa ODM Raila Odinga alipeleka kampeni zake za 'Azimio la Umoja' katika kaunti ya Murang'a.

Waziri huyo mkuu wa zamani alihutubia wakazi wa Mt Kenya katika uwanja wa Ihura katika juhudi za kuongeza kura zaidi kwenye kapu lake kutoka eneo hilo ambalo kwa miaka mingi limekuwa likimpinga.

Mamia ya wakazi walimiminika katika uwanja huo huku wasanii kadhaa maarufu wa eneo hilo wakiburudisha umati wa watu waliokuwa wamekusanyika.

Raila aliwaomba Wakenya kuwa na matumaini huku akiahidi kwamba mambo mazuri yaja hivi karibuni.

"Kenya inaungana. Wale wanaopinga umoja wa nchi wamekusanyika katika kona moja huku wengine tukiendelea kueneza amani na upendo nchini kote. Weka matumaini hai," alisema.

Mgombeaji huyo wa kiti cha urais katika chaguzi za mwezi Agosti aliandamana na viongozi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi pamoja na wengine kutoka eneo hilo la Mlima Kenya

Viongozi kutoka kaunti ya Muranga wakiongozwa na mwakilishi wa wanawake Sabina Chege, mbunge wa Mathioya Peter Kimari na mwenzake wa Gatanga Peter Nduati walimkabidhi Raila mapendekezo ya kaunti hiyo pamoja na viatu ambavyo walisema zingemsaidia kukwea mlima.

"Baba tunataka kukupatia memorandum ya kutoka kaunti ya Murang'a. Kisha tutakupatia viatu vya kukwea mlima. Mtampa baraka (akielekezea wakazi). Hizi viatu Baba, nataka uvichukue ni waterproof  utaweza kukwea mlima sawasawa. Mungu  akubariki na tunakuombea sana" Bi Chege alisema alipokuwa anamkabidhi Raila viatu hivyo.

Baada ya kinara wa ODM kupokea zawadi hiyo wahubiri waliokuwa wamehudhuria hafla hiyo walipiga  dua wakimtakia neema anapofanya kampeni zake katika eneo hilo.