"Hakuna matumaini ya upatanisho!" Mke wa gavana Hassan Joho awasilisha ombi la talaka

Muhtasari

•Bi Fazzini ameomba mahakama ya Kadhi kusuluhisha mzozo wa ndoa yao huku akisisitiza kwamba hakuna uwezekano wa kuifufua.

•Alisema walifunga ndoa mnamo mwezi Februari mwaka wa 2011 na wakaishi pamoja kama mke na mume kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kutengana kwao.

Gavana Ali Hassan Joho
Gavana Ali Hassan Joho
Image: MAKTABA

Kitumbua kimeonekana kuingia mchanga katika boma la gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho baada ya mke wake Madina Giovanni Fazzini kukimbilia mahakamani  kuwasilisha ombi la talaka.

Bi Fazzini ambaye amekuwa katika ndoa na gavana huyo wa muhula wa pili kwa kipindi cha takriban mwongo mmoja ameomba mahakama ya Kadhi kusuluhisha mzozo wa ndoa yao huku akisisitiza kwamba hakuna uwezekano wa kuifufua.

Katika barua yake, Fazzini alisema ndoa yao ilisambaratika mnamo mwaka wa 2013 na gavana Joho akagura nyumbani na kumwacha na watoto wawili. Alidai kuwa kwa sasa kila mmoja tayari amesonga mbele na maisha yake.

"Hakuna matumaini au uwezekano wa upatanisho au maelewano ya aina yoyote kati yangu na gavana," Ombi hilo lilisoma.

Fazzini aliwasilisha ombi hilo la talaka katika mahakama ya Kadhi ya Mombasa mnamo Januari 26 kupitia kampuni ya sheria ya Aziz M Ngare.

Katika ombi hilo, mama huyo wa watoto wawili alisema walifunga ndoa na naibu mwenyekiti huyo wa ODM mnamo mwezi Februari mwaka wa 2011 na wakaishi pamoja kama mke na mume kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kutengana kwao.

Baada ya mwanasiasa huyo kugura nyumba yake ndoa, Bi Fazzini ambaye anaaminika kuwa na asili ya Italia aliendelea kuishi pale pamoja na watoto hadi mwaka wa 2020 ambapo alihamia Malindi.

Fazzini amesisitiza kwamba hajashurutishwa na yeyote kuwasilisha kesi hiyo na amefanya hivyo kwa hiari yake mwenyewe.

Mahakama imempatia Joho siku kumi na tano kufika mahakamani na kuwasilisha majibu yake kuhusu kesi hiyo.