Martha Koome awakaripia mawakili Ahmednasir Abdullahi, Nelson Havi na Esther Ang'awa

Muhtasari

• Aliwataja mawakili Ahmednasir Abdullahi, Nelson Havi na Esther Ang'awa. Koome alisema Havi na Ang'awa waliandika jumbe kwenye mtandao wa Twitter kuhusu kesi hiyo mnamo Februari 15 na 19, 2022. 

Jaji mkuu Martha Koome
Image: Mahakama

Jaji Mkuu Martha Koome ameelezea kutofurahishwa na baadhi ya mawakili wakuu nchini kutokana na maoni yao kuhusu kesi ya rufaa ya BBI katika Mahakama ya Juu. 

Koome alisema maoni kama hayo yanaweza kuharibu taswira ya mahakama. "Wakati wa kuandika hukumu hii, mahakama ilizingatia kwa wasiwasi baadhi ya maoni yaliyotolewa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya mawakili, baadhi yao wakijitokeza katika kesi hii," Koome alisema. 

Aliwataja mawakili Ahmednasir Abdullahi, Nelson Havi na Esther Ang'awa. Koome alisema Havi na Ang'awa waliandika jumbe kwenye mtandao wa Twitter kuhusu kesi hiyo mnamo Februari 15 na 19, 2022. 

"Walipuuzilia mbali mahakama. Kwa mawakili kufika mbele ya mahakama kuu na kisha kuendelea kutoa taarifa zisizo za lazima, matusi na uvumi kuhusu hukumu zinazosubiriwa ni sawa na utovu wa maadili kwa upande wa wakili."

 Koome alizungumza muda mfupi kabla ya kutoa uamuzi wa Mahakama kuhusu rufaa ya BBI siku ya Alhamisi. Alisema yaliyomo kwenye mitandao ya kijamii, kuhusu mahakama, yalikusudiwa kushawishi, kutisha au kuichafua jina la mahakama. 

Koome alisema maoni hayo yanakwenda kinyume na vifungu vya Sheria ya Mawakili vinavyohusu mienendo isio na heshima inaoendana na hadhi ya mawakili. 

CJ alimkashifu Ahmednasir kutokana na msururu wa maoni aliyotoa kwenye twitter mnamo Februari 8 na 15 na Machi 29. 

Kulingana na Koome, maoni kama hayo yangefikia utovu wa nidhamu kitaaluma haswa kwa upande wa mawakili waliohusika katika kesi hiyo.

 "Kifungu cha 17 cha Sheria ya Mawakili kinazingatia cheo na hadhi ya mawakili waandamizi kwa misingi ya mienendo ya kitaaluma isiyoweza kutikisika," Koome alisema. 

Alisema sheria hiyo pia inawahusu mawakili wasiohusika katika kesi hiyo kwa vile wanafahamu kuwa hawaruhusiwi kutoa maoni yao katika masuala yaliyopo mahakamani. 

"Ni utaratibu ulioanzishwa vyema kwamba mawakili wanapaswa kujiepusha na moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kujaribu kushawishi mahakama isivyofaa kutoa uamuzi kwa njia moja au nyingine," Koome alisema. 

Maoni yake yaliunga mkono yale ya Jaji Smokin Wanjala aliyesema baadhi ya mawakili wamechukua hatua ya kuitishia mahakama kwa matumaini ya kuishawishi iamue kwa upande wao.