Mtu 1 amefariki na wengine kadhaa wajeruhiwa katika ajali ya barabarani Kwale

Dereva wa Matatu alipoteza miguu yake yote miwili na abiria wengine wanne kupata majeraha mabaya.

Muhtasari
  • Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota V8 Landcruiser na Nissan Matatu
  • Kulingana na chifu msaidizi wa eneo hilo Hamisi Mwavyoga, gari hilo aina ya Landcruiser lilikuwa likitoka Ukunda kuelekea Likoni huku matatu hiyo ikisubiri abiria ajali hiyo ilipotokea
Mtu 1 amefariki na wengine kadhaa wajeruhiwa katika ajali ya barabarani Kwale
Image: SHABAN OMAR

Mtu mmoja amefariki na wengine zaidi ya wanne wakiuguza majeraha mabaya kufuatia ajali mbaya ya barabarani katika makutano ya Kombani kaunti ya Kwale.

Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota V8 Landcruiser na Nissan Matatu.

Kulingana na chifu msaidizi wa eneo hilo Hamisi Mwavyoga, gari hilo aina ya Landcruiser lilikuwa likitoka Ukunda kuelekea Likoni huku matatu hiyo ikisubiri abiria ajali hiyo ilipotokea.

Mwavyoga alisema dereva wa Landcruiser alikuwa kwenye mwendo wa kasi sana aliposhindwa kuimudu na kugongana ana kwa ana na matatu ya stesheni.

"Landcruiser ilikuwa imeendeshwa kwa mwendo wa zaidi ya spidi ya 200 na ikagonga gombo la barabarani kabla ya kugonga matatu," alisema.

Dereva wa Matatu alipoteza miguu yake yote miwili na abiria wengine wanne kupata majeraha mabaya.

Walipoteza fahamu polisi walipowakimbiza katika hospitali ya kaunti ndogo ya Kwale.

Landcruiser ilikuwa imebeba abiria watano lakini ilikuwa na mikato midogo. Walikuwa na asili ya Kihindi.

Mmoja wa mashahidi alisema kuwa;

"Kulikuwa na magari saba tofauti yakija kwa mwendo wa kasi, kwa bahati nzuri madereva wa sita wa kwanza waliona gongo na kupunguza mwendo kidogo lakini Landcruiser ilifeli," alisema.

Juma alisema kutokana na breki ya papo hapo Landcruiser ilielea juu ya ardhi kabla ya kugonga matatu.

Aliyefariki alitambuliwa kuwa mkazi wa Likoni, kaunti ya Mombasa.

Mwamvyoga aliwashauri madereva wa magari kuepuka mwendo kasi.

"Endesha gari ukiwa na kiasi na uzingatie sheria za trafiki," alisema.

Siku mbili zilizopita, zaidi ya watu 20 walifariki katika ajali ya barabarani kwenye barabara kuu ya Taru-Samburu katika kaunti ndogo ya Kinango.