Mshtuko baada ya msimamizi wa uchaguzi wa Kirinyaga kuanguka na kufariki

Gitonga alisema kuwa mzee huyo wa miaka 57 hajawahi kulalamika kuhusu ugonjwa wowote.

Muhtasari

•Msimamizi wa uchaguzi wa kaunti ya Kirinyaga Jane Gitonga alisema afisa huyo alikuwa ameenda kuiona familia yake Nanyuki wikendi.

•Mwili wake umelazwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Nanyuki.

akitekeleza majukumu yake katika kituo cha kuhesabia kura eneo bunge mapema mwezi huu.
Msimamizi wa uchaguzi wa IEBC wa Gichugu Geoffrey Gitobu (Katika kitambulisho cha kijani kibichi, sweta na koti jeusi) akitekeleza majukumu yake katika kituo cha kuhesabia kura eneo bunge mapema mwezi huu.
Image: WANGECHI WANG'ONDU

Takriban wiki moja tu baada ya msimamizi wa uchaguzi wa Embakasi Mashariki Daniel Musyoka kupatikana amefariki kwenye kichaka karibu na mbuga ya kitaifa ya Amboseli,  pigo jingine limeikumba tume ya IEBC baada ya afisa mwingine kufariki kwa njia ya kutatanisha.

Afisa msimamizi wa IEBC wa eneo bunge la Gichugu Geoffrey Gitobu aliaga dunia siku ya Jumatatu baada ya kuugua kwa njia ya kutatanisha na kuzimia akiwa katika afisi ya IEBC ya Nanyuki.

Akizungumza kwa njia ya simu, msimamizi wa uchaguzi wa kaunti ya Kirinyaga Jane Gitonga alisema afisa huyo alikuwa ameenda kuiona familia yake Nanyuki wikendi baada ya zoezi kali la uchaguzi na alitakiwa kurejea Kirinyaga Jumatatu ili kujiandaa kurejea kazini mapema wiki hii.

"Nilikuwa nimemtuma apitie ofisini kwetu Nanyuki kunichapishia baadhi ya stakabadhi. Ni wakati huo ambapo alianguka kimaajabu akiwa ofisini hapo na kukutwa na umauti katika moja ya vituo vya afya vya kibinafsi vya Nanyuki ambako alikimbizwa. ,"alisema.

Gitonga alisema kuwa mzee huyo wa miaka 57 hajawahi kulalamika kuhusu ugonjwa wowote na kwa hivyo uchunguzi wa maiti ungefanywa ili kubaini chanzo cha kifo.

Alisema mwili wake umelazwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Nanyuki.