IEBC imetupatia idhini ya server moja pekee, sio nane- Orengo

Orengo alisema wamepewa idhini iliyodhibitiwa ya mitambo.

Muhtasari

•Orengo alisema wamemwandikia msajili kuhusu suala hilo na kuomba mahakama iingilie kati na kusaidia kutatua.

• Jaji Isaac Lenaola alimwambia kwamba walikuwa wakifahamu kinachoendelea.

Gavana wa Siaya James Orengo katika mahakama ya Juu mnamo Agosti 31,2022.
Gavana wa Siaya James Orengo katika mahakama ya Juu mnamo Agosti 31,2022.
Image: /DOUGLAS OKIDDY

Wakili mkuu James Orengo amedai kuwa tume ya IEBC imewaruhusu kufikia mtambo mmoja pekee wala sio nane.

Akitoa wasilisho lake Jumatano katika Mahakama ya Juu, Orengo alisema walikuwa wamepewa idhini iliyodhibitiwa ya mitambo.

"Tumepewa ufikiaji mdogo tu kwa matokeo yaliyotumwa. Na bado tunaelewa kuwa IEBC ina seva nane," alisema.

Orengo alisema wamemwandikia msajili kuhusu suala hilo na kuomba mahakama iingilie kati na kusaidia kutatua.

“Tumeandikia msajili ili mahakama isuluhishe hili,” alisema.

Kwa kujibu haraka, Jaji Isaac Lenaola alimwambia kwamba walikuwa wakifahamu kinachoendelea.

"Tunafahamu na tunalifuatilia, likitokea suala tutapokea ripoti kesho, zoezi lilikuwa limeanza na kulikuwa na suala la upatikanaji, tuendelee kesho," alisema.

Mahakama ya Juu ilimruhusu Raila Odinga kufikia mtambo wa teknolojia wa uchaguzi wa IEBC katika kile ambacho kingefanya au kuvunja kesi yake dhidi ya Rais mteule William Ruto.

Wakati huo huo, mgombea urais wa Azimio alishawishi mahakama ya upeo kuruhusu uchunguzi na kuhesabiwa upya kwa kura katika angalau vituo 15 vya kupigia kura.

Hii ni mara ya kwanza kwa mahakama kuu kuagiza kufunguliwa kwa masanduku ya kura za urais kwa ajili ya kuhesabiwa upya kura.

Raila alikuwa akiwania kiti cha urais kwa mara ya tano.

Alipinga kutangazwa kwa Ruto kama rais mteule na Wafula Chebukati, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.

Jaji wa Mahakama ya Upeo Isaac Lenaola alifafanua kwamba IEBC itawapa walalamishi "uwezo unaosimamiwa ambao sio wa kusoma pekee" kwa seva zake katika kituo cha kitaifa cha kuhesabia kura