Rigathi kumtuza mwanadada aliyembatiza jina 'Riggy G'

DP alisema alichukua jina hilo kwa nia njema kama njia ya kuwatia moyo vijana kama Chelimo.

Muhtasari

•Gachagua amesema kuwa tayari amekubali jina hilo alilopewa na mtumizi wa Twitter Ivy Chelimo kuwa lake.

•Ivy Chelimo anayejitambulisha kama  (@_chelimo_)  kwenye Twitter alikuwa mtu wa kwanza kutumia jina la utani la Riggy G.

Amesema kuwa tayari amekubali jina la utani 'Riggy G' ambalo alipewa na Ivy Chelimo.
Naibu rais Rigathi Gachagua. Amesema kuwa tayari amekubali jina la utani 'Riggy G' ambalo alipewa na Ivy Chelimo.
Image: MAKTABA

Naibu Rais Rigathi Gachagua anaonekana kufurahishwa sana na jina la utani alilopewa na wanamitandao 'Riggy G'.

Gachagua amesema kuwa tayari amekubali jina hilo alilopewa na mtumizi wa Twitter Ivy Chelimo kuwa lake.

"Mwanamke aliyeamua kuwa Rigathi Gachagua ni jina ngumu kiasi na halina muundo mzuri na kuona kwa kuwa nakaa mtu mzuri akanipa jina nzuri 'Riggy G', nilisema ni jina nzuri," alisema katika mahojiano na Citizen TV.

Mbunge huyo wa zamani wa Mathira alisema alichukua jina hilo kwa nia njema kama njia ya kuwatia moyo vijana kama Chelimo.

Pia alifichua kuwa ameomba kukutana na mwanadada huyo ili kushiriki chakula cha jioni pamoja naye na kujadiliana jinsi gani anaweza kusaidia kujenga maisha yake.

"Nimeambia wanangu watafute msichana huyo aje tushiriki chakula cha jioni pamoja naye. Nataka kumtia moyo msichana huyo. Nitaona nini naweza kumfanyia. Nitaangalia kama kutoka kwa mshahara wangu ninaweza kumuongezea nguvu kidogo ili aweze kufanya jambo  analotaka," alisema 

Ivy Chelimo anayejitambulisha kama  (@_chelimo_)  kwenye Twitter alikuwa mtu wa kwanza kutumia jina la utani la Riggy G kwenye mtandao huo wa kijamii mnamo tarehe 19 Julai 2022, mwendo wa saa 9.11PM.

Mnamo Septemba 13, Chelimo alialikwa katika ikulu ili kushiriki chakula cha mchana pamoja na viongozi wakuu na wageni wengine waalikwa baada ya rais na naibu wake kuapishwa katika uwanja wa Kasarani.