Wawili wafariki baada ya kunywa ethanol iliyoibwa kutoka kwa maabara ya shule Laikipia

Wengine wawili walikimbizwa hospitalini ambapo walitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Muhtasari

•Peter Kamitha ambaye alikuwa mpishi katika shule ya sekondari ya Il Polei na rafikiye Jane Naserian walifariki dunia katika Hospitali ya Nanyuki.

•Hillow alithibitisha kisa hicho na kusema kuwa uchunguzi umeanzishwa ili kubaini kilichosababisha vifo hivyo.

Rip
Rip
Image: HISANI

Watu wawili wamefariki katika eneo la Laikipia Kaskazini baada ya kunywa ethanol inayoaminika kuibwa kutoka kwa maabara ya shule ya upili ya eneo hilo.

Peter Kamitha 38 ambaye alikuwa mpishi katika shule ya sekondari ya Il Polei na rafiki yake Jane Naserian 32 walifariki dunia katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nanyuki (NTRH) siku ya Jumanne ambapo walikimbizwa na askari polisi walioitwa na chifu wa eneo hilo walipoanguka baada ya kunywa kinywaji hicho

Wanaume wengine wawili ambao pia walikunywa kinywaji hicho chenye sumu kali walikimbizwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Dol Dol, ambapo walitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Kamanda wa polisi wa Kaunti Ndogo ya Laikipia Kaskazini Ahmed Hillow alithibitisha kisa hicho na kusema kuwa uchunguzi umeanzishwa ili kubaini kilichosababisha vifo hivyo.

"Tulifanikiwa kupata robo lita ya kinywaji walichokuwa wakitumia na tumetuma sampuli kwa wanakemia wa serikali kwa uchambuzi zaidi na kujua yaliyomo halisi," Hillow alisema kwa simu.

Kamanda huyo wa polisi wa kaunti ndogo aliongeza kuwa kisa hicho kiliripotiwa na chifu msaidizi wa eneo hilo Richard Liasoi baada ya kufahamu kuwa wawili hao walikuwa wameanguka.

Aidha alisema kuwa maafisa wa upelelezi wanashuku huenda mpishi huyo aliiba kinywaji walichotumia shuleni ambako anafanya kazi ya upishi na kuamua kuwagawia marafiki zake kabla ya mkasa kutokea.

Hillow aliwaonya wakazi dhidi ya unywaji pombe haramu akibainisha kuwa ni hatari kwa afya, kwa kuwa haijatayarishwa katika viwango vya usafi na usalama vinavyopendekezwa.

Miili ya wawili hao imehifadhiwa katika hifadhi ya maiti ya NTRH ikisubiri uchunguzi wa baada ya maiti.

(Utafsiri: Samuel Maina)