Royal Media yavunja kimya baada ya mfanyikazi 1 kufariki kutokana na chakula chenye sumu

"Mawazo na sala zetu ziko pamoja na familia ya mfanyakazi wetu aliyefariki katika kipindi hiki kigumu."

Muhtasari
  • MD alisema wafanyikazi wengine kadhaa ambao waliathiriwa walikuwa wakifanya kazi kwenye zamu ya Krismasi

Royal Media Services imetoa taarifa kuhusu madai ya kuwekewa sumu kwenye chakula cha wafanyakazi wao.

Mkurugenzi Mtendaji Wachira Waruru alithibitisha kifo cha mfanyakazi mmoja akisema kampuni hiyo imesikitishwa na hali hiyo mbaya.

“Tumeshtushwa na kuhuzunishwa sana kuwafahamisha wananchi kuwa mtumishi mmoja amefariki kwa bahati mbaya kutokana na ugonjwa huo unaodhaniwa kuwa ni sumu kwenye chakula,” alisema.

"Mawazo na sala zetu ziko pamoja na familia ya mfanyakazi wetu aliyefariki katika kipindi hiki kigumu."

MD alisema wafanyikazi wengine kadhaa ambao waliathiriwa walikuwa wakifanya kazi kwenye zamu ya Krismasi.

"Kwa kuzingatia mipango ya kazi ya kipindi cha likizo, RMS ilishirikiana na kampuni ya kibinafsi ya upishi wa chakula ili kutoa chakula kwa wafanyakazi wanaofanya kazi wakati wa zamu ya Krismasi," alisema.

Waruru alisema mnamo Jumatatu, Desemba 26, baadhi ya wafanyikazi walilalamikia maumivu makali ya tumbo baada ya kula chakula kilichotolewa ndani ya majengo ya kampuni.

Aliongeza kuwa wafanyikazi kadhaa pia wamelazwa hospitalini kwa tuhuma za sumu.

"Tunatoa msaada unaohitajika kwa wafanyikazi walioathiriwa na tukio linaloshukiwa la sumu ya chakula kwa sasa linachunguzwa," alisema.

Mwandishi mwandamizi ni miongoni mwa waliolazwa katika hospitali hiyo.

Wengi wa wale waliokula chakula walilalamika kwa usumbufu wa tumbo.