Madaktari wasitisha mgomo uliokusudiwa ili kutoa fursa ya mazungumzo

Madaktari hao walikuwa wametishia kuondoa huduma ikiwa matakwa ya CBA yao ya 2017-2021 hayatatekelezwa.

Muhtasari
  • Walikashifu kukwama kwa utekelezaji wa makubaliano hayo na Wizara ya Afya, serikali za kaunti na mashirika ya umma katika sekta ya afya
Image: ANDREW KASUKU

Madaktari wamesitisha mgomo wao uliopaswa kuanza Ijumaa baada ya mashauriano na pande mbalimbali.

Madaktari hao walikuwa wametishia kuondoa huduma ikiwa matakwa ya CBA yao ya 2017-2021 hayatatekelezwa.

Katibu mkuu wa Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini Kenya Dkt Davji Atellah alisema hatua hiyo ni kutoa fursa ya mazungumzo.

Akizungumza katika afisi za muungano siku ya Alhamisi, Atellah alisema zaidi kuwa serikali imeonyesha kujitolea kushughulikia masuala hayo, ambayo yataangaliwa kabla ya Machi 5.

"Hatuko mbali na kuwa na makubaliano lakini tuko tayari kutoa nafasi ya mazungumzo,"alisema.

Muungano huo umekuwa katika mazungumzo na Waziri wa Afya Susan Wafula, kamati ya afya ya Baraza la Magavana na ile ya wafanyikazi katika juhudi za kuleta usawa na kuepusha mgomo huo.

Walikashifu kukwama kwa utekelezaji wa makubaliano hayo na Wizara ya Afya, serikali za kaunti na mashirika ya umma katika sekta ya afya.

Baadhi ya malalamiko yao ni pamoja na marekebisho ya mishahara, uundaji wa vyumba vya kupiga simu, kuajiriwa kwa wahitimu wasio na ajira, kupatiwa vitendea kazi na mashauriano ya mara kwa mara yatakayoleta maelewano ya viwanda.