Raila asitisha wito wa kususia gazeti la The Star

Raial alisema atwasilisha malalamishi yake kwa baraza la vyombo vya habari la Kenya

Muhtasari

• Raila siku ya Jumanne aliitisha kususiwa kwa gazeti la The Star akidai kuwa gazeti hilo halikuwa na usawa wa kusambaza habari.

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga akisoma gazeti la The Star.
Kiongozi wa Azimio Raila Odinga akisoma gazeti la The Star.
Image: MAKTABA

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga ameondoa wito kwa Wakenya kususia gazeti la The Star aliyotoa siku ya Jumanne.

Raila alisema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Alhamisi kwamba hatua hiyo ilifuatia mashauriano na washikadau.

"Tumekubali kusitisha ususiaji wetu wa gazeti la The Star. Badala yake, tumewasilisha malalamishi kwa Baraza la Vyombo vya Habari nchini Kenya kuhusu mapendeleo ya gazeti hilo," Raila alisema.

Raila siku ya Jumanne alitoa wito kwa Wakenya kususia gazeti la The Star pamoja mashirika mbali mbali, kwa kuegemea upande mmoja.

Hii ni licha ya Star kusalia kuwa huru, bila mapendeleo na lengo lake katika kuangazia pande zote za mgawanyiko wa kisiasa kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Wito huo wa kususia ulizua mjadala mkali nchini huku kukiwa na hofu kwamba hatua hiyo inaweza kuhatarisha maisha ya wanahabari.

Baraza la Vyombo vya Habari nchini Kenya, ilitoa taarifa yake kulaani hatua hiyo huku afisa mkuu mtendaji David Omwoyo akisema uhuru wa wanahabari ni haki muhimu inayowaruhusu wanahabari kuripoti matukio, masuala na watu bila hofu ya kuzuiwa au kukandamizwa.

"Mashambulizi kama haya yanadhoofisha uhuru wa vyombo vya habari na ni majaribio ya kudhoofisha jukumu la wanahabari katika kuwapa habari wapiga kura kulingana na maamuzi ya wahariri," Omwoyo alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa Radio Africa Group Patrick Quarcoo alitoa taarifa na kulaani matamshi hayo dhidi ya The Star na kusema kuwa hayafai na hayana msingi.

Quarcoo alisema katika miaka yake 15 ya kuwepo, Star haijaegemea upande wowote katika uandishi wake wa matukio ya kisiasa kote nchini na imepokea tuzo kwa ajili ya malengo yake kwa miaka mingi.