Odinga anaharibu mali ya watu ndio tuketi, haiwezekani! - DP Gachagua

"Haitatokea tena. Yeye akae kwake, si ako na wajukuu, akae huko…” Gachagua alisema.

Muhtasari

• Alisema kwamba Odinga alifanya hivyo kipindi cha rais hayati Moi akaitwa kwa maridhiano, akafanya hivyo wakati wa marais wengine waliofuata pia akaitwa lakini safari hii hatofaulu.

DP Gachagua amuomba Odinga kusitisha maandamano.
DP Gachagua amuomba Odinga kusitisha maandamano.
Image: Facebook, Maktaba

Naibu wa rais Rigathi Gachagua amekanusha madai ya baadhi ya viongozi wa upinzani kwamba yeye ndiye kizingiti kikuu katika upatanishi baina ya rais Ruto na kinara wa Azimio, Raila Odinga.

Gachagua akizunguza Alhamisi alisema kwamba yeye hajazuia kitu chochote ila anachokipinga ni kwamba haiwezekani Odinga atake maridhiano ya amano baada ya kuvuruga na kuharibu mali za watu katika maandamano ya Jumatatu.

“Ati wanasema ati mimi ndio nakataa, mimi sikatai chochote, kile mimi nasema ni ati mtu aharibu mali ya watu ndio tumuite? Haiwezekani,” naibu rais alisema.

Gachagua alidai kwamba si mara ya kwanza Odinga Anajaribu mbinu hiyo lakini safari hii atavuna mabua kwani haitowezekana hata kidogo.

Alisema kwamba Odinga alifanya hivyo kipindi cha rais hayati Moi akaitwa kwa maridhiano, akafanya hivyo wakati wa marais wengine waliofuata pia akaitwa lakini safari hii hatofaulu.

Naibu rais alimtaka kutulia kwake pamoja na wajukuu wake.

“Alifanya hivyo kwa Moi akaitwa, akafanya hivyo kwa Kibaki akaitwa, akaja akafanya hivyo tena kwa Uhuru, akaitwa tena, haitatokea tena. Yeye akae kwake, si ako na wajukuu, akae huko…” Gachagua alisema.

Jumatano baadhi ya viongozi wa upinzani wakiongozwa na naibu gavana wa Kakamega Ayub Savula wakisema kwamba Ruto ameonesha dalili zote za kutaka maridhiano na Odinga lakini naibu wake Gachagua ndiye amekuwa akiweka vikwazo vingi, huku akisema kwamba vigezo vyake vitaendelea kuathiri Wakenya wengi ambao wanategemea biashara.

Odinga alisema kwamba maandamanao yatakuwa yanafanyika kila siku ya Jumatatu na Ahamisi hadi pale serikali ya Ruto itaridhia kuwasikiliza na kutekeleza matakwa yao.

Baadhi ya matakwa ambayo Odinga anadai ni kufunguliwa kwa seva za IEBC, kusitishwa kw mchakato wa kuwateua makamishna wapya wa IEBC, kupunguzwa kwa gharama ya maisha miongoni mwa mengine.