Serikali yataka mataifa ya kigeni kumwekea Raila vikwazo kwa kuzua rabsha nchini

Serikali ilidai kuwa maandamano yaliyosababishwa na Raila yalileta hasara nchini

Muhtasari

• Raila alitangaza kuwa maandamano itakuwa kila  Jumatatu na Alhamisi.

Odinga amtambua Ruto kama rais
Odinga amtambua Ruto kama rais
Image: Facebook

Utawala wa Rais William Ruto umeyaandikia mataifa ya kigeni kuwawekea vikwazo- ikiwa ni pamoja na kuwawekea vikwazo vya kusafiri viongozi wa Azimio.

Serikali inashtumu upinzani kwa kuvuraga amani nchini kutokana na maandamano ya kila wiki na kukataa kutambua uongozi wa rais William Riuto. 

Katika barua ya kina kutoka kwa Wizara ya Masuala ya Kigeni, serikali inamshutumu kiongozi wa Azimio Raila Odinga kwa kupanga kumpindua Rais William Ruto. Wizara hiyo inasema kuwa hatua ya Raila siku ya Jumatatu ililenga kumtimua Ruto kama Rais aliyechaguliwa kikatiba na kutaka kujitangaza rais kinyume na sheria.

Serikali inashikilia kuwa mwito wa Raila wa maandamano nchini kote wakati Serikali mpya inakaribia miezi sita madarakani na inafanya kazi kwa bidii kufufua uchumi, hayana msingi.

Serikali inasema maandamano hayo si ya amani kama inavyodaiwa lakini yamekithiri uharibifu wa mali na miundo mbinu.

Wizara inasema hatua ya Raila na viongozi wenzake kutishia kuvamia ikulu ya rais ni sawa na kitendo cha uhaini.

Raila Jumatatu aliandaa maandamano makubwa yaliyolemaza shughuli katika kaunti za Nairobi na Kisumu na ametoa wito kufanyika kwa maandamano zaidi mara mbili kwa wiki ili kushinikiza serikali kupunguza gharama ya maisha.

Kulingana na barua hiyo, maafisa wa usalama waliwazuia waandamanaji hao kuingia katikati mwa jiji na Ikulu. 

"Licha ya vizuizi vya polisi, baadhi ya waandamanaji waliharibu na kupora mali ambayo thamani yake itabainishwa katika siku zijazo," serikali ilisema kwenye barua hiyo.