(Picha) Dennis Okari alivyoacha kamera na kukimbilia maisha yake wakati wa maandamano 2017

Okari alipakia picha Jumatatu wakati wa maandamano ya Azimio, alikumbuka jinsi alichana mbuga kuokoa maisha yake 2017 maji yalipozidi unga.

Muhtasari

• Okari kipindi hicho akifanya kazi na NTV alitumwa kupeperusha ripoti moja kwa moja kutoka nyanjani.

• Lakini maandamano hayo yaligeuka uwanja wa mapambano baina ya polisi na waandamanaji.

Dennis Okari akikimbilia maisha yake baada ya maandamano kugeuka vurugu.
Dennis Okari akikimbilia maisha yake baada ya maandamano kugeuka vurugu.
Image: Facebook,

Jumatatu taifa la Kenya lilikumbwa na msukosuko kwa mamia ya waandamanaji kujitokeza katika baadhi ya miji kushiriki maandamano ambayo yaliitishwa na kinara wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga.

Katika maandamano hayo, wanahabari wengi haswa wapiga picha walionekana katika mstari wa mbele kabisa wakihakikisha kwamba hakuna tukio lililopita pasi na kuoneshwa kwenye runinga ambazo zilikuwa zinapeperusha maandamano hayo moja kwa moja.

Aliyekuwa mwanahabari wa NTV, Dennis Okari baada ya kufuatilia maandamano hayo, safari hii akiwa nje ya jumba la habari, amekumbuka jinsi alijipata katikati mwa zogo baina ya maafisa wa kukabili waandamanaji na waandamanaji wenyewe katika mfarakano uliozuka pindi baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Okari kipindi hicho akiitumikia runinga ya NTV, alitwikwa jukumu la kuhakikisha matukio yote yangepeperushwa moja kwa moja kutoka nyanjani ambapo polisi walikuwa wanakabiliana na waandamanaji.

Mwanahabari huyo alisema kwamba baada ya maandamanao hayo kuchacha na kuvuka mipaka, yaligeuka na kuwa uwanja wa mapambano baina ya polisi na waandamanaji, huku wanahabari wakijipata katikati mwa zogo hilo.

Okari kwa kuhofia maisha yake aliacha kamera ikiwa bado inaendelea kupeperusha matukio moja kwa moja na kukimbilia maisha yake katika kile alikiita ‘miguu niponye’.

“Siku ndefu ya waandishi wa habari. Mimi wakati wa 2017. Nikipeperusha moja kwa moja ripoti kuhusu maandamano halafu......mguu niponye,” Okari aliandika kwenye picha hizo za kumbukumbu.

Katika picha hizo tatu alizozipakia baada ya kushuhudia kile wanahabari wenza walikuwa wanapitia katika maandamano ya Raila Odinga mwaka huu, Okari anaonekana akiwa na wanahabari wengine.

Kisha ghafla katika picha ya pili anaonekana akichana mbuga huku mkononi akiwa na kipaza sauti pekee na picha ya tatu anaonekana akirudisha macho nyuma bila kuamini kile alichokiona.