Eric Omondi akamatwa na polisi akielekea Ikulu

Ni mara ya tatu mcheshi huyo kukamatwa na polisi kwa kujaribu kuandamana

Muhtasari

• Omondi alitaka kumpa Rais William Ruto CV hizo ili kumuonyesha jinsi ukosefu wa kazi ulivyokuwa tatizo nchini.

Mchekeshaji Eric Omondi siku ya Jumanne alikamatwa tena akielekea Ikulu ya rais.

Eric alikuwa akivuta mkokoteni aliyodai kuwa ulikuwa na maelfu ya stakabadhi za vijana wanaotafuta kazi.

Dhamira yake kuu ilikuwa ni kuziwasilisha Ikulu. Wakati akivuta mkokoteni wake, mcheshi huyo pia alikosoa serikali kwa kutobuni nafasi za kazi kwa mamilioni ya Wakenya.

Omondi alitaka kumpa Rais William Ruto wasifu kazi hizo ili kumuonyesha jinsi ukosefu wa kazi ulivyokuwa tatizo nchini.

  "Sitaki kuweka maisha ya watu hatarini. Nilikusanya CV milioni tatu ambazo napeleka kwa Mhe William Ruto ili aone jinsi watu wake wameenda chuo kikuu lakini hawana kazi. "

Hata hivyo, alikamatwa katika Barabara Kuu ya Uhuru na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Central. Omondi alikuwa ameapa kuendelea kushinikiza serikali kukabiliana na gharama ya juu ya maisha lakini alitumai kuwa ghasia hizo hazitasumbua.

Alisema anachotaka ni serikali kusikiliza kilio cha wananchi. Mchekeshaji huyo katika wiki chache zilizopita amekamatwa mara mbili na kushtakiwa mara moja kwa kuvuruga amani kupitia mkutano usio halali.

Alikamatwa kwa mara ya kwanza mnamo Februari 21 pamoja na wengine 17 alipokuwa akiongoza maandamano ya kupinga gharama ya maisha. Mnamo Machi 1, alikamatwa tena alipokuwa akisambaza unga kwa Wakenya katika uwanja wa City Stadium. Kesi inayohusiana na kukamatwa kwa mara ya kwanza ilisukumwa Jumatatu hadi Mei.