Wakili Ombeta awatetea wanandoa waliorekodiwa wakiiba kondoo wa Uhuru Kenyatta

Wanandoa hao walionekana wakijaribu kumweka kondoo mmoja ndani ya gari lao.

Muhtasari

•Kulingana na wakili Ombeta, wanandoa hao hawakuwa wakiiba kondoo yule bali walikuwa wakimsaidia kuvuka barabara.

•Makumi ya watu wasiojulikana walivamia ardhi inayomilikiwa na familia ya Kenyatta karibu na Eastern Bypass, Ruiru, na kuharibu mali.

Image: HISANI

Wakili Cliff Ombeta ametaka hatua kutochukuliwa dhidi ya wanandoa ambao walinaswa kwenye kamera wakidaiwa kuiba kondoo katika shamba la familia ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta, katika eneo la Ruiru, kaunti ya Kiambu.

Siku ya Jumatatu, kundi la watu wasiojulikana walivamia shamba la familia ya Kenyatta la Northlands, wakaharibu mali, kukata miti kadhaa na hata kuiba idadi isiyojulikana ya mifugo. Baadhi ya matukio ya uvamizi huo yalinaswa kwenye kamera na picha na video zikasambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Wanandoa walionekana wakijaribu kumuweka kondoo mmoja ndani ya gari lao lililokuwa limeegeshwa barabarani na Wakenya kwenye mitandao wamekuwa wakitoa maoni tofauti kuhusu video hiyo inayovuma. Baadhi wamekuwa wakiwashutumu wawili hao kwa kuiba na kuwakosoa huku wengine wakiwatetea.

Kulingana na wakili Ombeta, wanandoa hao hawakuwa wakiiba kondoo yule bali walikuwa wakimsaidia kuvuka barabara.

"Huu sio wizi. Wanamuokoa kondoo aliyepotea ambaye alikuwa akirandaranda kwenye barabara hatari na yenye shughuli nyingi. Kwa kweli walikuwa wamemuacha  salama tu," Ombeta alisema kwenye mtandao wa Twitter.

Wakili huyo pia alibainisha kwamba kondoo huyo hakunaswa kwenye video akiwa ndani ya gari ya wanandoa hao.

Awali siku ya Jumanne, wakili mwenzake Ombeta, Donald B. Kipkorir alitumia ukurasa wake maarufu wa Twitter kuwakosoa wanandoa hao.

"Baada ya kuiba mbuzi kutoka Northlands ya Kenyatta, **** na mkewe watawaambia nini watoto wao? Watasema nini watakapoenda kanisani Jumapili? Picha hii itawaandama milele. Mbuzi mmoja akisimamisha maisha yako milele," aliandika.

Jumatatu, Makumi ya watu wasiojulikana walivamia ardhi inayomilikiwa na familia ya Kenyatta karibu na Eastern Bypass, Ruiru, na kuharibu mali.

Watu hao ambao walikuwa na misumeno ya umeme na mapanga walikata miti kadhaa kabla ya kutoroka na idadi isiyojulikana ya kondoo kutoka hapo.

Hii ni baada ya wao kuvunja uzio kuzunguka shamba hilo kubwa.

Walioshuhudia walisema genge hilo lilipata ufikiaji wa ardhi hiyo kutoka upande wa Kamakis kupitia njia yenye shughuli nyingi na wengine walionekana wakiwa wamebeba kondoo kutoka kwa mali hiyo.