Serikali iliondoa usalama wangu ila sitaomba wairudishe-Asema Raila

Kiongozi huyo wa upinzani alibainisha kuwa hatakwenda kortini kurejesha usalama wake.

Muhtasari

•Akizungumza Jumatano, Raila alisema ,hataomba  serikali kurejesha usalama wake kwa sababu ana haki ya kulindwa kisheria, kama Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Kenya.

•"Waliondoa usalama wangu na hawajaurudisha. Sitajisumbua kuwakumbusha au kulalamika lakini unavyojua usalama wangu uko katika Sheria na unakubaliwa na sheria,"

Raila Odinga
Raila Odinga
Image: Facebook

Kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga sasa anasema kuwa serikali iliondoa usalama wake miezi mitatu iliyopita, na hawajarudisha. 

Akizungumza Jumatano, Raila alisema, hataomba  serikali kurejesha usalama wake kwa sababu ana haki ya kulindwa kisheria, kama Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Kenya.

"Waliondoa usalama wangu na hawajaurudisha. Sitajisumbua kuwakumbusha au kulalamika lakini unavyojua usalama wangu uko katika Sheria na unakubaliwa na sheria," Raila alisema 

Katika mahojiano na KTN News  aliongeza kuwa;

"Ni busara kwa serikali au rais,kufahamu kwamba wapo kwa sababu ya majukumu yangu kama Waziri Mkuu wa nchi hii. Nina haki ya kupata malipo ya kustaafu na usalama ni sehemu yake lakini sitajisumbua kuwaomba."

Kiongozi huyo wa upinzani alibainisha kuwa hatakwenda kortini kurejesha usalama wake.

Alisema itakuwa ni kupoteza muda wake kwa madai kuwa mahakama imenyakuliwa na serikali inajua ni kwa nini waliamua kuondoa walinzi wake.

"Wanajua wao ndio waliowachukua, kwanini waulize? Wakitaka kuzirudisha watazirudisha," alisema.

Akijibu swali, ikiwa labda amewasilisha ombi lilote kwa serikali kurudisha usalama wake alisema,

"Kwa kweli, unapendekeza niende kuomba kwamba warudishe usalama. Wana sababu zao kwa nini waliondoa usalama wangu na ikiwa sababu hizo hazipo tena watazirudisha."

Raila alisema ana imani kuwa Mungu anamlinda, ndio maana jambo la kuwaondoa walinzi wake halimsumbui na kusema kwamba usalama wake mkubwa unatoka kwa wananchi.

"Ninajali usalama wangu na ninaamini kuwa kuna mtu huko juu ambaye ananiangalia kwa hivyo sisumbuki. Lakini usalama wangu mkubwa ni watu ndio maana naweza kuzunguka barabarani bila shida,"  alisema. .

Raila ni miongoni mwa viongozi ambao usalama wao uliondolewa na serikali wakati wa maandamano ya kila wiki dhidi ya serikali.

Serikali lilidai kuwa viongozi hao walikuwa wakitumia vibaya walinzi hatua iliyofanya waondolewe.