Niondolee kesi kama ulivyoahidi-Miguna Miguna amwambia Rais Ruto

Miguna alirejea Kenya kutoka Kanada Oktoba 20, 2022 wiki baada ya Rais Ruto kuchukua mamlaka.

Muhtasari
  • Miguna alifurushwa kutoka nchini mnamo Februari 2018 na serikali ya Jubilee baada ya kuzuiliwa kwa siku kadhaa
  • "Mnamo Januari, Rais William Ruto aliniomba msamaha kwa mateso ya kinyama, kulazimishwa uhamishoni na kutendewa vibaya na serikali ambayo alihudumu kama Naibu Rais. Aliahidi kuwa kesi zote zinazohusiana na dhuluma hizo zitatatuliwa. Miezi 12 baadaye, 'bado nasubiri," 
MIGUNA MIGUNA AOMBA RAIS KUONDOA KESI YAKE KAMA ALIVYOAHIDI
MIGUNA MIGUNA AOMBA RAIS KUONDOA KESI YAKE KAMA ALIVYOAHIDI

Wakili Miguna Miguna amemtaka Rais William Ruto kutimiza ahadi aliyompa walipokutana baada ya kurejea nchini.

Miguna alifurushwa kutoka nchini mnamo Februari 2018 na serikali ya Jubilee baada ya kuzuiliwa kwa siku kadhaa.

Alirejea mwezi mmoja baadaye lakini alifanyiwa vurugu kwenye uwanja wa ndege na kufurushwa kwa mara ya pili.

Wakili huyo alifichua kuwa Ruto alipoingia mamlakani, alimwomba msamaha kwa mateso ambayoserikali ya Jubilee ilimfanyia na kuahidi kuondoa mashtaka yote ambayo yalikuwa yameelekezwa kwake.

Kupitia akaunti yake ya X Miguna alimshutumu Rais Ruto kwa kukosa kutimiza ahadi yake miezi 12 baadaye.

"Mnamo Januari, Rais William Ruto aliniomba msamaha kwa mateso ya kinyama, kulazimishwa uhamishoni na kutendewa vibaya na serikali ambayo alihudumu kama Naibu Rais. Aliahidi kuwa kesi zote zinazohusiana na dhuluma hizo zitatatuliwa. Miezi 12 baadaye, 'bado nasubiri," Miguna alisema

Katika chapisho lingine, wakili huyo alithibitisha kuwa alitii amri ya  aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani Fred Matiangi, wito wa mahakama na maombi nyumbani kwake Karen.

"Leo, Mhudumu wangu aliwasilisha Wito na Mashauri ya Mahakama katika HCCC 163 ya 2019 kwa Fred Okeng'o MATIANG'I katika jumba lake la kifahari huko KCB Karen Ngong Estate," alichapisha. Aliongeza: "Matiang'i na washtakiwa wengine lazima wajibu kwa mateso, matumizi mabaya ya mamlaka, mashtaka mabaya, uhamisho wa kulazimishwa na uhalifu mwingine mwingi. Haki itapatikana bila kujali itachukua muda gani."

Wakili huyo alisisitiza kuwa mahakama kuu imeamua ukweli wa tuhuma alizowasilisha licha ya mshtakiwa kushindwa kuwasilisha taarifa ya utetezi.

"Washitakiwa hawajawasilisha maelezo ya utetezi, maana yake ni kushindwa, pili, Mahakama Kuu tayari imewaona wanawajibika. Maana kinachosubiriwa ni tathmini ya uharibifu," alifafanua.

Wakili Miguna Miguna  alikamatwa siku chache baada ya kumwapisha Raila Odinga kama rais wa wananchi katika bustani ya Uhuru  mnamo Januari 10.

Mnamo Februari 7, 2018, alifukuzwa nchini  baada ya polisi kushindwa kumwasilisha mahakamani.

"Hata kama mtu alikuwa na nia ya kunifukuza popote kwa sababu zozote zile, kuna taratibu za kisheria zilizowekwa vyema ambazo lazima zifuatwe na haki za kimsingi zinapaswa kuzingatiwa, ambazo Matiang'i amekiuka," ilisema taarifa ya Miguna

Miguna alirejea Kenya kutoka Kanada Oktoba 20, 2022 wiki baada ya Rais Ruto kuchukua mamlaka.

Alishukuru juhudi za rais katika kurahisisha safari yake. 

"Bila utawala huu, nisingerudi nyumbani. "Rais William Ruto, Rais wa Jamhuri ya Kenya na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi mapema leo asubuhi aliniomba radhi kwa niaba yake na  kwa niaba ya Serikali kwa unyama niliofanyiwa na utawala uliopita,” alisema