Kwa nini Miguna Miguna anamtaka Eliud Kipchoge kustaafu baada ya kushinda Berlin Marathon

“Hongera sana Eliud Kipchoge. Umeweka historia. Sasa, staafu ukiwa juu! Viva!” Miguna Miguna aliandika.

Muhtasari

•Miguna alitoa ushauri huo kwa Kipchoge alipokuwa akimpongeza kwa kushinda taji lake la tano la Berlin Marathon.

•Miguna alibainisha kuwa Kipchoge tayari ameweka historia kubwa na kumtaka aondoke jukwaani akiwa bado kileleni.

amemtaka Eliud Kipchoge kustaafu riadha
Wakili Miguna Miguna amemtaka Eliud Kipchoge kustaafu riadha
Image: HISANI

Wakili maarufu wa Kenya Miguna Miguna amemshauri bingwa wa mbio za marathon Eliud Kipchoge kustaafu kutoka kwa riadha.

Miguna alitoa ushauri huo kwa mshikilizi huyo wa rekodi ya dunia ya marathon alipokuwa akimpongeza kwa kushinda taji lake la tano la Berlin Marathon mnamo Jumapili, Septemba 24.

Katika ujumbe wake za pongezi, mshauri huyo wa kisiasa wa zamani wa kinara wa ODM Raila Odinga alibainisha kuwa Kipchoge tayari ameweka historia kubwa na kumtaka aondoke jukwaani akiwa bado kileleni.

“Hongera sana Eliud Kipchoge. Umeweka historia. Sasa, staafu ukiwa juu! Viva!” Miguna Miguna aliandika kwenye mtandao wa Twitter.

Kipchoge ambaye sasa ana umri wa miaka 38 alishinda mbio za Berlin Marathon kwa mara ya tano siku ya Jumapili baada ya kumaliza mbio hizo kwa saa 2:02:42. Ushindi huo ulimfanya kuwa mwanariadha wa kwanza kushinda Berlin Marathon mara tano.

Mwanariadha huyo Mkenya ndiye anayeshikilia rekodi ya dunia ya marathon kwa sasa, ambayo aliweka baada ya kumaliza kwa muda wa 2:01:09.

Kabla ya mbio za Berlin Marathon 2023, Kipchoge alisema kuwa lengo lake kuu ni kushinda medali tatu za dhahabu za Olimpiki mfululizo na kwamba anaamini kukimbia mjini Berlin ndiyo njia bora ya kujiandaa kwa mafanikio hayo.

Kipchoge alishinda taji lake la kwanza la ubingwa wa dunia mwaka wa 2003 kwa kushinda mbio za vijana katika Mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika na kuweka rekodi ya dunia ya vijana zaidi ya mita 5000 kwenye mbio hizo.

Akiwa na umri wa miaka kumi na minane, alikua bingwa wa dunia wa mita 5000 katika Mashindano ya Dunia ya 2003 akiwa na rekodi ya ubingwa, kisha akashindia Kenya shaba ya Olimpiki mnamo 2004 na shaba kwenye Mashindano ya Ndani ya Dunia ya 2006.

Kipchoge alitwaa medali za fedha katika Mashindano ya Dunia ya 2007, Olimpiki ya Beijing ya 2008 na Michezo ya Jumuiya ya Madola ya 2010.