Polisi wetu hawataenda kufanyiwa majaribio Haiti-kindiki

Kindiki alisema Kenya imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono misheni ya amani kote ulimwenguni

Muhtasari

•  Akiwa mbele ya Kamati ya Utawala na Usalama wa Kitaifa siku ya Alhamisi, Waziri huyo alisema polisi wa Kenya wametumwa kwa shughuli za amani nje ya nchi mara kadhaa.

Waziri wa usalama Kithure Kindiki akifika mbele ya Kamati ya Utawala na Usalama wa Kitaifa Oktoba 12, 2023. Picha: MINA
Waziri wa usalama Kithure Kindiki akifika mbele ya Kamati ya Utawala na Usalama wa Kitaifa Oktoba 12, 2023. Picha: MINA

  Waziri wa usalama na  maswala  ya Ndani Kithure Kindiki ametetea mipango ya kutuma maafisa wa polisi nchini Haiti akisema Kenya inajulikana kimataifa kwa kushiriki katika misheni za amani.

Akiwa mbele ya Kamati ya Utawala na Usalama wa Kitaifa siku ya Alhamisi, Waziri huyo alisema polisi wa Kenya wametumwa kwa shughuli za amani nje ya nchi mara kadhaa.

Alizitaja nchi ambazo maafisa wa polisi wa Kenya wamehudumu zikiwemo  Namibia, Sudan Kusini, Sudan,  Somalia, Bosnia na Herzogovina. "Hatutumi maafisa wetu kama nguruwe",alisema waziri Kindiki.

Kenya imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono harakati za amani kote ulimwenguni sio na wanajeshi tu bali pia kitengo cha polisi," alisema.

Kindiki aliambia kamati inayoongozwa na Mbunge wa Narok Magharibi Gabriel Tongoyo kwamba timu hiyo inajumuisha maafisa kutoka Huduma ya Kitaifa ya Polisi na Wizara ya Masuala ya Kigeni.

Alisema ujumbe huyo ambao imerejea, ilikwenda kutathmini uwezekano wa misheni hiyo.

"Tutatuma timu nyingine kwa Umoja wa Mataifa kwa misheni ya kidiplomasia. Waziri wa Mambo ya Nje ataongoza ujumbe huo," aliongeza.

Mahakama ilizuia kwa muda serikali kupeleka mamia ya maafisa wa polisi nchini Haiti katika misheni iliyoidhinishwa na Umoja wa Mataifa yenye lengo la kusaidia taifa la Haiti kukabiliana na ghasia za magenge.

Amri ya mahakama iliyotolewa Jumatatu ni halali hadi Oktoba 24,Jaji Chacha Mwita alisimamisha kutumwa kwa polisi hadi kesi iliyowasilishwa na Thirdway Alliance na Wakenya wawili isikizwe.

Waliteta kuwa uamuzi wa kupeleka maafisa wa polisi nje ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki ni kinyume cha sheria.

Mnamo Julai, Kenya iliahidi kutoa maafisa 1,000 wa polisi baada ya Haiti kuomba usaidizi wa kimataifa na maafisa wa usalama kusaidia katika vita vyake dhidi ya magenge yanayolaumiwa kwa kuchochea ghasia.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa takriban raia 200,000 wa Haiti wamekimbia makwao kutokana na  ghasia zinazozidi kuongezeka, huku magenge yenye silaha yakitekeleza mauaji ya kiholela, utekaji nyara, ubakaji na kuchoma nyumba za watu.