Watahiniwa Wa KCPE kujua shule watakazojiunga nazo kuanzia wiki ijayo - Machogu

Machogu alisema mwaka huu mwanafunzi aliyeongoza amepata alama 428. Aidha, alisema ni watahiniwa wawili tu waliohusika katika wizi wa mitihani.

Muhtasari

• Machogu alisema zoezi la upangaji wa nafasi hao litafanyika kwa muda wa wiki mbili.

• "Upangaji wa wanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza utaanza Jumatatu nakudumu kwa kipindi cha wiki mbili ili kuwapa wazazi wakati wakujipanga,"

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu na Katibu wa Idara ya Elimu ya Msingi Belio Kipsang
Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu na Katibu wa Idara ya Elimu ya Msingi Belio Kipsang
Image: HISANI

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amesema zoezi la upangaji wa kidato cha kwanza kwa watahiniwa wa KCPE litaanza Jumatatu, Novemba 27.

Machogu alisema zoezi la upangaji wa nafasi hao litafanyika kwa muda wa wiki mbili.

"Upangaji wa wanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza utaanza Jumatatu nakudumu kwa kipindi cha wiki mbili ili kuwapa wazazi wakati wakujipanga," CS alisema.

Alizungumza Alhamisi katika nyumba ya Mtihani ambapo alitoa matokeo ya KCPE ya 2023.

Machogu alisema mwaka huu mwanafunzi aliyeongoza amepata alama 428. Aidha, alisema ni watahiniwa wawili tu waliohusika katika wizi wa  mitihani.

"Mmoja alikuwa na matini wakati mwingine  akiwa na simu ya rununu," alisema.

Waziri alisema watahiniwa 8523 walipata alama 400 na zaidi ikilinganishwa na mwaka jana ambapo watahiniwa 9443 walipata zaidi ya 400.

Alisema wanafunzi waliopata alama kati ya 300 na 399 waliwakilisha asilimia 24.94 ya jumla ya watahiniwa.

Hii ilikuwa ni wanafunzi 352,782 huku idadi ya watahiniwa ikiwa 307,756 mwaka 2022.

Machogu alisema wanafunzi 658,278 walipata kati ya alama 200 na 299.

Kati ya alama 100 na 199 kulikuwa na watahiniwa 383,025. Wakati kati ya alama 1 na 99, kulikuwa na watahiniwa 2060.

Watahiniwa 9354 walishindwa kufanya mtihani wa KCPE 2023.

Machogu alisema watapata nafasi ya pili Januari.