Watu 76 wafariki kutokana na mafuriko, serikali yatenga B. 7

Msemaji wa Ikulu Hussein Mohammed alibaini kuwa serikali imetenga Ksh.7 bilioni kushughulikia athari za mvua.

Muhtasari

• Sehemu ya pesa hizo ikulu ilisema, ni za wafugaji wa ng'ombe wa maziwa huku serikali ikichukua hatua ya kununua maziwa ya ziada.

Mama aanguka kutoka kwa boda boda.
Mama aanguka kutoka kwa boda boda.
Image: TikTok

Takriban Wakenya 76 wamefariki kutokana na mvua inayoendelea ya El Nino ambayo imesababisha maafa kote nchini na kusababisha mafuriko na maporomoko.

Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed alisema kuwa Baraza la Mawaziri, katika kikao cha dharura siku ya Jumatatu kilichoongozwa na Rais William Ruto kilikuja na hatua kadhaa za kusaidia kupunguza athari za El Nino kwa Wakenya.

Haya yanajiri kufuatia mafuriko ambayo yamesababisha vifo vya watu, familia kuhama na kuharibu mali.

Kulingana na taarifa ya baraza la mawaziri jumla ya  kaunti ya 38 kati ya 47 ziko katika hali ya hatari kukumbwa na mafuriko, mito kupasua kingo zake, maporomoko ya ardhi, kupoteza mifugo na uharibifu wa mashamba na miundombinu.

"Baraza la Mawaziri lilisikitika kwamba tumepoteza Wakenya 76 kwa El Nino huku nyumba 35,000 zikihama maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni Kaskazini Mashariki, Mashariki na Mikoa ya Pwani."

Msemaji wa Ikulu pia alibaini kuwa serikali imetenga Ksh.7 bilioni kushughulikia athari za mvua.

Sehemu ya pesa hizo ikulu ilisema, ni za wafugaji wa ng'ombe wa maziwa huku serikali ikichukua hatua ya kununua maziwa ya ziada.

"Ili kusaidia wakulima ambao wameathiriwa vibaya, serikali imesambaza shilingi 500 milioni kwa kampuniya KCC Mpya ili kununua maziwa ya ziada katika msimu huu wa mvua," alisema.