EACC yapata idhini ya DPP kumfungulia kesi Seneta Mandago kuhusiana na sakata ya elimu

EACC imekuwa ikichunguza mpango wa ufadhili wa Shilingi bilioni 1.1 ulioanzishwa na serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu wakati wa enzi ya Mandago.

Muhtasari

• Akaunti ya Uasin Gishu Overseas Education Trust Fund inasemekana kufunguliwa Mei 2021 na maafisa watatu waliotajwa kuwa watia saini.

Mkurugenzi Mtendaji wa EACC Twalib Mbarak wakati wa kikao na wanahabari katika Kaunti ya Murang'a mnamo Desemba 8, Picha: Alice Waithera
Mkurugenzi Mtendaji wa EACC Twalib Mbarak wakati wa kikao na wanahabari katika Kaunti ya Murang'a mnamo Desemba 8, Picha: Alice Waithera

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi sasa inataka seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago kushtakiwa kwa sakata ya ufadhili wa masomo ya Ufini. 

Mkurugenzi Mtendaji wa EACC Twalib Mbarak amesema tume hiyo imepokea kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kumfungulia mashtaka seneta huyo. Mbarak ambaye alikuwa akizungumza katika Kaunti ya Murang’a wakati wa kongamano la kujumuika na umma kabla ya Siku ya Kimataifa inayoadhimishwa Desemba 9 alibainisha kuwa tume hiyo imepata ushahidi utakaotumiwa dhidi ya gavana huyo wa zamani. 

"Tumependekeza afunguliwe mashtaka na tumepokea kibali kutoka kwa DPP kwa sababu tumepata kitu kumhusu," alisema. 

EACC imekuwa ikichunguza mpango wa ufadhili wa Shilingi bilioni 1.1 ulioanzishwa na serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu wakati wa enzi ya Mandago. Fedha hizo zilikusanywa kutoka kwa wazazi ili kuwezesha mpango wa ufadhili wa masomo kwa watoto wao kwenda Ufini na Kanada.

Akaunti ya Uasin Gishu Overseas Education Trust Fund inasemekana kufunguliwa Mei 2021 na maafisa watatu waliotajwa kuwa watia saini. Akaunti hiyo inadaiwa kupokea jumla ya Shilingi 837,855,889 kati ya Mei 2021 na Desemba 2022 kutoka kwa wanafunzi zaidi ya 200 waliosafiri kwenda Finland kusomea kozi mbalimbali katika taasisi mbalimbali.Fedha hizo zilitakiwa kutumwa kwa taasisi za masomo kutoka kwenye akaunti. 

Rekodi zinaonyesha kuwa Chuo Kikuu cha Tampere kilipokea Shilingi 113,750,634 huku Chuo Kikuu cha JAMK kikipata Shilingi 657,500, Chuo Kikuu cha Northern Lights kikipata Shilingi 5,023,480 na Chuo Kikuu cha Elimu kikipokea Shilingi 3,249,220. Chuo Kikuu cha LUT kilipokea Sh6,552,000, SCI Stenberg kilipokea Sh7,570,500, Chuo cha Ubora cha Edu kilipokea Sh145,816,300 na Chuo cha Eton Vancouver kikipokea Sh2,196,000. 

Takriban wanafunzi 202 walitumwa Ufini kati ya Septemba 2021 na Septemba 2022 kati yao 67 walikubaliwa katika Chuo Kikuu cha Laurea kusomea shahada ya uuguzi.Kundi jingine la wanafunzi 25 lilikubaliwa katika Chuo Kikuu cha Jyvaskylla kusomea uuguzi huku wanafunzi 111 wakijiunga na Chuo Kikuu cha Tampere. Kila mwanafunzi alikuwa amechangia Shilingi milioni 1.19  za karo za shule kwa hazina hiyo kabla ya kwenda Finland na Shilingi 100,000 zaidi za tikiti za ndege. Sh80,000 za ziada zilichangwa kwa malazi ya miezi mitatu na Sh30,000 kwa bima. 

Hata hivyo, baadhi ya vyuo vikuu vinadaiwa kutopokea fedha zinazohitajika hivyo kuwaweka wanafunzi hao katika hatari ya kufukuzwa. Chuo kikuu kimojawapo kinadaiwa kusitisha makubaliano yake na serikali ya kaunti.