"Lazima ifike mwisho!" Raila avunja kimya kuhusu ongezeko la mauaji ya wanawake

Raila aliomba hatua za haraka zichukuliwe akitaja kesi hizo za kusikitisha kuwa kama dharura ya kitaifa.

Muhtasari

•Wanawake kadhaa wameripotiwa kufariki kwa njia isiyoeleweka huku miili ya baadhi ya wahasiriwa ikipatikana katika hali mbaya.

•"Janga baya la mauaji ya wanawake sasa ni dharura ya kitaifa. Ni tishio kwa usalama wa nchi. Lazima ifike mwisho,” Raila alisema.

 

akihutubia waandishi wa habari.
Kiongozi wa ODM Raila Odinga akihutubia waandishi wa habari.
Image: MAKTABA

Kinara wa ODM Raila Odinga amelaani mauaji ya wanawake kufuatia ongezeko kubwa ya visa hivyo nchini.

Katika wiki kadhaa zilizopita, wanawake kadhaa wameripotiwa kufariki kwa njia isiyoeleweka huku miili ya baadhi ya wahasiriwa ikipatikana katika hali mbaya.

Katika taarifa yake siku ya Jumatano asubuhi, kiongozi huyo wa muungano wa Azimio la Umoja alisema ongezeko la mauaji ya wanawake linatia wasiwasi sana na akasema kwamba vitendo kama hivyo havipaswi kuruhusiwa kuendelea.

"Inasikitisha kuona ongezeko la kuhuzunisha la vifo vya wanawake vijana, na kuacha majonzi kwa familia na marafiki," Raila alisema katika taarifa kwenye akaunti yake ya Twitter.

Aliongeza, "Jambo lisilo la kawaida la mauaji haya haliwezi kuwa kawaida mpya. Mauaji ni na yatakuwa mabaya siku zote, na hakuna kisingizio.”

Raila aliomba hatua za haraka zichukuliwe kukomesha mauaji ya wanawake vijana akitaja kesi hizo za kusikitisha kuwa kama dharura ya kitaifa.

"Janga baya la mauaji ya wanawake sasa ni dharura ya kitaifa. Ni tishio kwa usalama wa nchi. Lazima ifike mwisho,” alisema.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya mshukiwa kukamatwa kuhusiana na mauaji ya hivi majuzi ya mwanadada mwenye umri wa miaka 20 katika mtaa wa TRM Drive, Roysambu.

Siku ya Jumanne, wapelelezi walikuwa wakimhoji mwanamume wanayeamini kuwa alimuua mwanamke huyo ambaye mwili wake ulipatikana umekatwakatwa na kutupwa katika pipa la takataka jijini Nairobi.

Inasemekana mshukiwa alinaswa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta alipokuwa akijaribu kutoroka nchini.

Alizuiliwa akisubiri kutambuliwa na kuhojiwa, chanzo cha polisi kiliambia Radio Jambo.

"Ni mapema mno kusema kama yeye ndiye mtu anayesakwa kuhusu mauaji au la. Inabidi tusubiri,” afisa mmoja wa polisi alisema.

Mshukiwa alizuiliwa katika uwanja wa ndege kabla ya timu ya maafisa kutoka Kasarani na makao makuu ya DCI kumchukua ili kuhojiwa.

Viungo na mikono ya mwanamke huy zilipatikana zimekatwakatwa na kuwekwa kwa karatasi ya plastiki na kufungwa kwenye shuka la kitanda.