70% ya wanafunzi tayari wamejiunga na kidato cha kwanza

Machogu alisema wizara itashirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani kufanya msako wa kila nyumba ili kuafikia sera ya mpito ya silimia 100

Muhtasari

• Wizara ya Elimu kupitia Jomo Kenyatta Foundation (JKF) na Equity Group Foundation imetoa misaada ya masomo 9,000 kwa wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Kwanza.

akizungumza alipoongoza utoaji wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka Wakfu wa KCB mtaani Karen, Nairobi Januari 17, 2023.
Waziri wa elimu, Ezekiel Machogu akizungumza alipoongoza utoaji wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka Wakfu wa KCB mtaani Karen, Nairobi Januari 17, 2023.
Image: LEAH MUKANGAI

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amebainisha kuwa hadi asilimia 70 ya Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza kote nchini wameripoti kwa shule zao.

Waziri alitoa hakikisho kwamba wizara itafanya kila juhudi kuhakikisha wanafunzi zaidi ya milioni 1.4 waliofanya mtihani wa KCPE wa 2023 wanajiunga na shule walizopangiwa.

“Wizara hadi sasa imefurahishwa na zoezi linaloendelea ambapo zaidi ya asilimia 70 ya wote waliopangiwa shule za sekondari wamesharipoti,” alisema.

Waziri alizungumza Jumatano alipoongoza utoaji wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 1,000 kutoka Wakfu wa KCB kwa wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na shule za upili.

Machogu alisema wizara itashirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa kufanya msako wa nyumba hadi nyumba ili kufikia asilimia 100 ya wanafunzi kujiunga na sekondari kutoka shule za msingi.

Aidha, Machogu alibainisha kuwa Wizara ya Elimu kupitia Jomo Kenyatta Foundation (JKF) na Equity Group Foundation imetoa misaada ya masomo 9,000 kwa wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Kwanza.

Walionufaika na ufadhili huo walitoka Kaunti zote 47. Ni wanafunzi wasiojiweza na walio katika mazingira magumu na ambao walipata alama 280 na zaidi katika Mtihani wa KCPE wa 2023.

"Ili pawepo usawa watahiniwa wenye mahitaji maalum na ulemavu ambao walipata chini ya alama 280 pia walinufaika," Machogu alisema.

Waziri alisema wanafunzi kutoka katika Vikundi vilivyo katika Mazingira Hatari na Waliotengwa na walifikisha alama 250 na zaidi pia walizingatiwa.

"Napenda kuwahimiza washirika wengine wa elimu kuingilia kati na kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wetu wenye uhitaji ili kuhakikisha tunafikia sera ya mpito ya asilimia 100 na hakuna mtoto yeyote anayesalia nyuma katika mfumo wetu wa elimu," alisema.

Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza walianza kuripoti katika shule za sekondari kote nchini kuanzia Jumatatu na mchakato wa uandikishaji utafanyika hadi Ijumaa.

Mtihani wa mwisho wa KCPE 2023 chini ya mtaala wa 8-4-4 ulishuhudia idadi kubwa zaidi ya watahiniwa katika historia ya mtihani huo nchini.

Watahiniwa 1,233,852 walifanya mtihani wa kitaifa mwaka wa 2022. Idadi hiyo ilipanda hadi 1,406,557 mwaka wa 2023.