Hakuna uhasama baina ya Ruto na Gachagua, baadhi ya viongozi Mt. Kenya wasema

Mbunge wa Kipipiri, Wanjiku Muhia, amesema wawili hao wameungana kikamilifu katika utekelezaji wa manifesto za kampeni.

Muhtasari

• Viongozi hao walikanusha madai kuwa serikali ya Kenya Kwanza imegawanyika akinyooshea upinzani kidole kwa kueneza uvumi huo.

Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua
Image: ANDREW KASUKU

Baadhi ya viongozi wa eneo la Mlima Kenya wamesisitiza kuwa hakuna mtafaruku kati ya Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua vile imekuwa ikidaiwa na wengi.

Akizungumza na Gazeti la Star, Mbunge wa Kipipiri, Wanjiku Muhia, amesema wawili hao wameungana kikamilifu katika utekelezaji wa manifesto za kampeni na vilevile kuwaunganisha Wakenya kutoka pande zote za kisiasa.

Alibainisha kuwa chama cha UDA na jamii yote ya Kenya Kwanza kwa sasa wanalenga kuunga mkono serikali katika utekelezaji na uboreshaji wa ajenda za maendeleo.

Hivi majuzi Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga alikariri maoni sawa na hayo, akisisitiza kuwa eneo la Mlima Kenya litaendelea kuwa na umoja katika kumuunga mkono Rais Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua.

"Watu wa Mlima Kenya wanaunga mkono kwa dhati William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua. Wanathamini watu waaminifu na watalipa kila wakati kwa kujitolea kwao kwa manufaa yao. Sioni mabadiliko yoyote katika Urais,” alisema Kahiga.

Alisisitiza haja ya kuunga mkono utawala uliopo kwa ukuaji endelevu na kuwataka wananchi kuipa serikali muda wa kutosha kutimiza ahadi zake.

Mbunge wa Gatanga Edward Muriu alikariri maoni sawa na hayo akibainisha kuwa serikali ya Kenya Kwanza kwa sasa imeungana na haitayumbishwa katika kutekeleza kile walichowaahidi Wakenya.

Aliwataka Wakenya kuunga mkono serikali ya sasa akibainisha kuwa kwa sasa wanarekebisha makosa ambayo yalifanywa na utawala uliopita ukiongozwa na Uhuru Kenyatta.

"Tunalenga kutimiza manifesto za kampeni na Wakenya wanapaswa kuunga mkono serikali," Muriu alisema.

Alikanusha madai kuwa serikali ya Kenya Kwanza imegawanyika akinyooshea upinzani kidole kwa kueneza uvumi huo.

MCA wa Kiamwangi Kung'u Smart aidha amesema Wakenya wanapaswa kuipa serikali muda wa kutosha wa kutoa huduma badala ya kuikosoa kila siku.

Alisema kuwa siasa za urithi zisiwe kipaumbele akiwataka viongozi kueneza umoja.

"Sisi kama viongozi tunapaswa kukumbatia umoja na kuunga mkono serikali katika ngazi ya kitaifa na katika Kaunti kwa ajili ya wapiga kura waliotuchagua mamlakani," Kung'u alisema.