Rais William Ruto aomboleza kifo cha rais mustaafu wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi

Rais Samia Suluhu alitangaza kuwa Mwinyi atazikwa Machi 2, 2024, Ugunja maeneo ya nyanda za juu za Zanzibar.

Muhtasari

• Rais wa Tanzania Samia Suluhu alitangaza kifo cha Mwinyi Alhamisi jioni akisema alikata roho jioni mwendo wa saa kumi na unusu.

Marehemu Rais mstaafu wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi.
Marehemu Rais mstaafu wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi.
Image: PCS

Rais William Ruto ameomboleza kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu alitangaza kifo cha Mwinyi Alhamisi jioni akisema alikata roho jioni mwendo wa saa kumi na unusu.

Katika taarifa yake kwa mtandao wa X, Ruto alimtaja Mwinyi kama kiongozi mkuu mwenye kumbu kumbu nzito.

"Natoa pole zangu na za wananchi wa Kenya kwa Rais Samia Suluhu na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha Mh. Ali Hassan Mwinyi - Rais wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunaungana katika kuomboleza kifo cha Mhe. kumpoteza kiongozi mkuu ambaye kumbu kumbu zake nzito hazitafifia,” alisema.

"Pumzika kwa Amani Mzee Mwinyi."

Rais huyo wa zamani aliugua saratani ya mapafu.

Rais Suluhu alitangaza kuwa Mwinyi atazikwa Machi 2, 2024, Ugunja maeneo ya nyanda za juu za Zanzibar.

Alikuwa Rais wa Tanzania kati ya 1985 hadi 1995.

Mwinyi alichukua nafasi ya rais mwanzilishi wa Tanzania Julius Nyerere.

Alikuwa akipokea dawa katika Hospitali mjini London kabla ya kurejea Tanzania ambako aliendelea na matibabu.

Rais Suluhu ametangaza kipindi cha siku 7 cha maombolezo ambapo bendera zitapandishwa nusu mlingoti.

"Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, natuma salamu za rambirambi kwa familia, marafiki na wananchi wa Tanzania kwa msiba huu mkubwa," alisema.

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga na mkewe Ida pia waliomboleza aliyekuwa Rais Mwinyi.

"Mimi na Mama Ida tunatoa pole kwa Rais Samia Suluhu kwa kuondokewa na Mh. Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunaungana na Taifa la Tanzania katika maombolezo ya kiongozi mkuu na mwananchi wa Afrika," Raila alisema.

"Apumzike kwa Amani."