KDF, Mabadiliko yatangazwa katika uongozi wa jeshi la Kenya

Naibu mkuu mpya wa majeshi sasa ni Meja Jenerali Charles Muriu Kahariri ambaye alipandishwa cheo hadi Luteni Jenerali

Muhtasari

• Mabadiliko hayo yalitangazwa kufuatia mkutano wa kitengo cha juu cha maamuzi katika jeshi.

• Kamanda wa Jeshi la nchi kavu Luteni Jenerali Peter Mbogo Njiru pia alistaafu baada ya kutimiza umri wake wa kustaafu.

• Rais William Ruto pia amempandisha cheo Brigedia Thomas Njoroge Ng'ang'a hadi cheo cha Meja Jenerali na kumteua kuwa Kamanda wa kikosi cha Wanamaji wa Kenya.

pamoja na maafisa wengine wakuu wa jeshi wakati wa mkutano wa Alhamisi. Picha: HISANI
Waziri wa Ulinzi Aden Duale akiwa na Mkuu wa Majeshi Jenerali Francis Ogolla pamoja na maafisa wengine wakuu wa jeshi wakati wa mkutano wa Alhamisi. Picha: HISANI

Idara ya jeshi imetangaza mabadiliko katika usimamizi wa idara hiyo huku  Naibu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Lt Jenerali Jonah Mwangi akistaafu.

Kamanda wa Jeshi la nchi kavu Luteni Jenerali Peter Mbogo Njiru pia alistaafu baada ya kutimiza umri wake wa kustaafu.

Naibu mkuu mpya wa majeshi sasa ni Meja Jenerali Charles Muriu Kahariri ambaye alipandishwa cheo hadi Luteni Jenerali huku Meja Jenerali David Kimaiyo Tarus akichukua nafasi ya Kamanda wa Jeshi la nchi kavu.

Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Kenya Meja Jenerali Jim Mutai alipandishwa cheo hadi Luteni Jenerali na kuhamishwa hadi Chuo cha Ulinzi kama Naibu Chansela wa Chuo cha Kitaifa cha Ulinzi.

Mabadiliko hayo yalitangazwa kufuatia mkutano wa kitengo cha juu cha maamuzi katika jeshi.

Baraza la Ulinzi lilikutana Alhamisi chini ya uenyekiti wa Waziri wa Ulinzi Aden Duale na kufanya mabadiliko hayo.

Walimjulisha Rais William Ruto kama Amiri Jeshi Mkuu kuhusu makubaliano yao kabla ya kuyaweka hadharani.

Rais pia amempandisha cheo Brigedia Thomas Njoroge Ng'ang'a hadi cheo cha Meja Jenerali na kumteua kuwa Kamanda wa kikosi cha Wanamaji wa Kenya.

Hadi kuteuliwa kuwa Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Kenya alikuwa Kamanda wa kambi ya wanamaji ya Manda.

Luteni Jenerali Njiru aliteuliwa kushikilia wadhifa huo mwaka wa 2022 kuchukua nafasi ya Luteni Jenerali Walter Koipaton ambaye alistaafu baada ya kutumikia muhula wake wa miaka minne.

Meja Jenerali Nganga anatoka Jeshi la Wanamaji la Kenya na kwa mujibu wa sheria, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi atatoka katika Jeshi la Wanamaji la Kenya ikiwa na Jenerali Francis Ogolla atakapostaafu mwaka ujao.

Jenerali Ogolla anaweza kuongezewa muda ofisini kwa mwaka mmoja ikiwa Baraza la Ulinzi ambalo yeye ni mwanachama litashauri hivyo.

Mabadiliko mengine yaliyofanywa ni pamoja na Meja Jenerali Juma Shee Mwinyikai aliyepandishwa cheo na kuwa Luteni Jenerali na kuteuliwa kuwa kamanda wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi na Meja Jenerali Mohamed Nur Hassan aliyeteuliwa kuwa Naibu Kamanda wa Jeshi la nchi kavu.

Brigedia Luka Kipkemoi Kuto alipandishwa cheo na kuwa Meja Jenerali na kuteuliwa kama Afisa Mkuu wa Kamandi ya Mashariki huku Meja Jenerali Aphaxard Muthuri Kiugu akitumwa katika chuo cha kijeshi na kutajwa kama kamanda.

Brig Peter Shikuku Chelimo aliteuliwa kuwa naibu kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Kenya huku Brig Yahya Abdi akiteuliwa kuwa mkurugenzi mkuu wa wafanyikazi wa Jeshi la Kenya katika Chuo cha Kitaifa cha Ulinzi.

Chini ya sheria zilizoletwa na aliyekuwa Mkuu wa majeshi Jenerali Mstaafu Daudi Tonje - zilizopitishwa na kujulikana kama Sheria za Tonje – wadhifa wa mkuu wa majeshi unazungushwa kati ya vikosi vitatu.

Hawa ni Jeshi la nchi kavu, Jeshi la Anga na Jeshi la Wanamaji la Kenya. Jenerali Ogolla anatoka katika Jeshi la Wanahewa la Kenya na mtangulizi wake, Jenerali Robert Kibochi, alikuwa kutoka Jeshi la nchi kavu. Hii ina maana kwamba mkuu wa majeshi atakayefuata lazima atoke katika Jeshi la Wanamaji la Kenya.