Imefichuliwa: Kwa nini polisi wa trafiki walipuuza vikao vya jopo la Maraga

Jopo hilo limependekeza kuvunjwa kwa Kitengo cha trafiki na badala yake kuweka Kitengo cha Kudhibiti Trafiki (TCU).

Muhtasari

• Maafisa wote wa kitengo cha sasa cha trafiki na wale ambao wamehudumu hapo awali wasipelekwe kwenye TUC mpya au majukumu au shughuli zozote za usimamizi wa trafiki. 

Afisa wa polisi wa trafiki akikagua matatu Picha: MAKTABA
Afisa wa polisi wa trafiki akikagua matatu Picha: MAKTABA

Hakukuwa na uwasilishaji rasmi wa Kitengo cha Polisi wa Trafiki wakati wa vikao vya umma na vya wadau vilivyoendeshwa kote nchini na Kikosi Kazi cha Kitaifa kuhusu mageuzi ya polisi.

Ripoti kutoka kwa kikosi kazi hicho inafichua kuwa ni afisa mmoja tu wa polisi wa trafiki aliyeshiriki katika mojawapo ya mikutano ya kaunti.

"Jopo hilo lilikagua ripoti za mikutano ya hadhara, na kupokea memoranda kutoka kwa washikadau wakuu, ikiwa ni pamoja na NTSA... Jopo hata hivyo, lilibainisha kuwa hapakuwa na maoni yoyote ya Kitengo cha trafiki," inasema.

Ingawa kamati haijatoa maelezo yoyote kwa nini maofisa hao walipuuza vikao hivyo, inaaminika kwamba dhana ya rushwa iliyokithiri ambayo imekuwa ikitawala kitengo hicho inaweza kuwa imechangia.

Kulingana na jopo kazi hilo , kulikuwa na maoni “mazito" kutoka kwa washiriki kuhusu ufisadi unaohusishwa na polisi wa trafiki.

Washiriki wanasemekana kutaja kunyanyaswa kwa madereva wanaokataa "kushirikiana" na maafisa wa trafiki kwenye barabara za umma.

"Mfano ulitajwa wa waendesha pikipiki au boda boda kote nchini," ripoti hiyo inasema.

Inabainisha kuwa wakati pikipiki nyingi zinazuiliwa kwa misingi halali, nyingi zaidi zinazuiliwa kwa kushindwa kutoa hongo kwa maafisa wa trafiki.

Hali hii imesababisha mrundikano wa pikipiki katika vituo vingi vya polisi kote nchini kwa mashtaka ya uwongo dhidi ya waendeshaji na madereva wengine wa magari.

Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Ufisadi katika Huduma ya Polisi wa 2016 unakiri kuwepo kwa ufisadi ulioenea katika idara ya trafiki.

Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei aliitisha mkutano wa makamanda wa polisi wakiwemo wakuu wa trafiki mjini Nairobi Septemba mwaka uliyopita katika jitihada za kutafuta suluhu la ufisadi uliokita mizizi katika idara ya polisi.

"Ni kutokana na hili ambapo Rais ameniagiza nifanye mkutano huu nanyi na tufanye majadiliano ya wazi kuhusu jinsi ya kumaliza ufisadi na kusafisha huduma," Koskei alisema.

Kamati hiyo inayoongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga ilifahamishwa wakati wa mikutano yake kuwa kukithiri kwa hongo barabarani kumesababisha kuanzishwa kwa vizuizi vya barabarani ambavyo huwa karibu kila mara.

Vizuizi vya barabarani husimamiwa na kitengo cha trafiki cha eneo fulani na kamanda wa kituo hicho, ripoti inasema.

"Ilibainika kuwa mara nyingi, kamanda wa kituo hutoa gari rasmi la kituo, ambalo kwa kawaida huegeshwa kwenye kizuizi cha barabarani na hutumika kusaidia katika ukusanyaji wa rushwa badala ya kutekeleza majukumu mengine muhimu," ripoti inaongeza. 

Huko Busia, kwa mfano, ripoti hiyo inabainisha kuwa wanachama wa jopo kazi waliona wakati wa ziara za mashinani kwamba kulikuwa na kizuizi cha barabarani cha polisi kila baada ya kilomita 10. 

Ni kutokana na hali hiyo ambapo kamati iliyoongozwa na Jaji mstaafu David Maraga imependekeza kuvunjwa kwa Kitengo hicho na badala yake kuweka Kitengo cha Kudhibiti Trafiki (TCU). TUC itafanya kazi kwa kuzingatia mfumo uliojumuishwa na wa kiotomatiki wa udhibiti wa trafiki. 

Pia inataka maafisa wote walio chini ya kitengo cha sasa na wale ambao wamehudumu hapo awali wasipelekwe kwenye TUC mpya au majukumu au shughuli zozote za usimamizi wa trafiki.