KQ yarejesha safari za ndege Kinshasa

KQ ilisitisha safari zake za ndege hadi Kinshasha, ikisema kuwa haingeweza kutoa huduma ipasavyo bila wafanyikazi wake.

Muhtasari

• Afisa Mkuu Mtendaji wa KQ Allan Kilavuka alikariri kuwa wafanyikazi wao hawana hatia.

• Kulingana na PS, Lydia Mbotela, meneja wa KQ anayefanya kazi DRC, aliachiliwa baada ya mazungumzo yaliyosimamiwa na Mwambata wa Kijeshi wa Kenya na Balozi Mdogo.

Ndege ya Kenya Airways
Image: MAKTABA

Shirika la ndege la Kenya Airways siku ya Jumatatu lilitangaza kurejesha safari za ndege kuelekea Kinshasa baada ya mfanyakazi aliyekuwa amezuiliwa huko kuachiliwa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa KQ Allan Kilavuka alikariri kuwa wafanyikazi wao hawana hatia katika sakata iliyosababisha kusimamishwa kwa safari za ndege kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

“Tunataka kusisitiza kwamba wafanyakazi wetu hawana hatia na walikuwa wakitekeleza majukumu yao kwa kufuata taratibu zilizowekwa. Tunasimama na kutokuwa na hatia na tutaendelea kuwaunga mkono.”

"Kwa usaidizi unaohitajika, tuna furaha kutangaza kwamba Shirika la Ndege la Kenya Airways litarejesha safari za ndege hadi Kinshasa tarehe 8 Mei 2024. Tunatazamia kuwahudumia wateja wetu kwa mara nyingine," alisema.

Kusitishwa kwa safari za ndege kuelekea DRC kumeathiri vibaya shughuli nyingi nchini humo.

Mfanyakazi wa shirika la ndege la Kenya Airways ambaye alikuwa amezuiliwa na Kitengo cha Ujasusi cha Kijeshi cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hatimaye aliachiliwa Jumatatu baada ya kuzuiliwa kwa wiki mbili.

Katibu Mkuu wa Masuala ya Kigeni Korir Sing'oei alitangaza hayo Jumatatu jioni baada ya mazungumzo.

Kulingana na PS, Lydia Mbotela, meneja wa KQ anayefanya kazi DRC, aliachiliwa baada ya mazungumzo yaliyosimamiwa na Mwambata wa Kijeshi wa Kenya na Balozi Mdogo.

"Ninashukuru sana kufahamisha kwamba Lydia Mbotela, Meneja wa KQ nchini DRC, ameachiliwa hivi punde na mamlaka mjini Kinshasa," Sing'oei aliandika kwenye jukwaa la kijamii la X siku ya Jumatatu.

Kilavuka alisema wawili hao walikamatwa na Kitengo cha Ujasusi cha Kijeshi huko Kinshasa kwa "kukosa hati za forodha za shehena ya thamani."

Kwa upande mwingine, Kilavuka alikashifu mamlaka ya Kinshasa kwa kuwakamata wawili hao akidai kuwa walikuwa wakishikiliwa kinyume na amri ya mahakama na kwamba shehena inayohusika haijakubalika na KQ.

Huku hali ikizidi kuzorota, KQ ilisitisha safari zake za ndege hadi Kinshasha, ikisema katika taarifa kuwa haingeweza kutoa huduma zake ipasavyo bila wafanyikazi wake.

Kilavuka aliwashukuru wafanyikazi wa Wizara ya Masuala ya Kigeni wakiongozwa na Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi kwa juhudi zao zilizofanikisha kuachiliwa huru.