Mbunge Kitany ndiye Mwasilishaji wa hoja ya kunishtaki - CS Linturi

Linturi anakabiliwa na mashtaka matatu ya madai ya utovu wa nidhamu, ukiukaji mkubwa wa katiba na kutenda uhalifu.

Muhtasari

• Alisema kesi zote mahakamani kati ya Linturi na Ketany o zimetolewa uamuzi kuegemea upande wa mteja wake.

• Wamboka alisema ilikuwa ni bahati mbaya kwa Waziri huyo kuendelea kumvuta katika kila jambo ilhali ana familia yake.

Waziri wa Kilimo Mithika Linturi na wakili wake Muthomi Thiankolu Picha: EZEKIEL AMING'A
Waziri wa Kilimo Mithika Linturi na wakili wake Muthomi Thiankolu Picha: EZEKIEL AMING'A

Waziri wa Kilimo na Mifugo Mithika Linturi amedai kuwa mbunge wa Aldai Marianne Kitany ndiye aliyechangia hoja ya kutimuliwa kwake.

Wakili wa Linturi Muthomi Thiankolu aliambia Kamati Teule ya bunge inayomchunguza waziri kwamba ni Kitany wala si Mbunge wa Bumula Jack Wamboka ambaye ndiye aliyehusika na ombi la mteja wake kung'atuka.

"Mwasilishaji wa Hoja hii ni Mbunge wa Aldai," Thiankolu alisisitiza.

Kitany na Linturi waliwahi kuwa katika uhusiano kabla ya kuachana.

Wamboka aliwasilisha hoja ya kuondolewa ofisini kwa waziri ambayo Bunge la Kitaifa liliidhinisha Mei 2.

Linturi anakabiliwa na mashtaka matatu ya madai ya utovu wa nidhamu, ukiukaji mkubwa wa katiba na kutenda uhalifu.

Katika mawasilisho yake, Thiankolu aliambia kamati inayoongozwa na Naomi Waqo kwamba shtaka la pili lililetwa na tofauti kati ya Linturi na Mbunge wa Aldai.

“Ni mizozo ya kibinafsi kati ya Linturi na Mbunge wa Aldai. Swali la kuu ni; jinsi gani mtoa hoja alifanya tofauti kati ya wawili hawa kama msingi mkuu ambao madai ya pili yamewekwa?” Thiankolu aliongeza.

Alisema kesi zote mahakamani kati ya wawili hao zimetolewa uamuzi kuegemea upande wa mteja wake.

"Mtu alipoteza kesi katika mahakama kuu ya rufaa, mahakama zote za mahakimu na kisha akafanya kesi hizi kuwa msingi wa shtaka namba mbili," aliongeza.

Aliongeza kuwa DCI ilichunguza tuhuma za mbunge huyo dhidi ya Waziri na kupeleka faili hizo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ambaye alisema zilifungwa.

"DPP alifunga mambo haya yote Mei 31 mwaka jana," alisema.

Akitoa maoni yake, Wamboka ameambia Linturi kutomuingiza mbunge wa Aldai katika sakata ya kuondolewa madarakani.

Huku akiwasilisha kesi yake ya kutaka Waziri huyo afutwe mbele ya kamati maalum ya wanachama 11, Wamboka alisema inasikitisha kwamba Waziri huyo alimtumia mbunge huyo kujibu barua yake.

"Nimeangalia majibu ya CS na haiko mbali na barua ya mapenzi ya mpenzi aliyejawa na hasira," alisema.

"Haya ni mambo mazito ya kupunguzwa kwa mambo ya wapenzi," alisema.

"Ukiachwa achika," alisema.

Wamboka alisema ilikuwa ni bahati mbaya kwa Waziri huyo kuendelea kumvuta katika kila jambo ilhali ana familia yake.