Mapenzi ya Linturi na Kitany yatawala vikao vya kamati maalum

Mwakilishi wa Wanawake wa Busia Catherine Omanyo aliiomba kamati hiyo kumwalika Kitany kufika mbele ya kamati.

Muhtasari

• Mbunge wa Matuga Kassim Tandaza alibainisha kuwa kwa sababu mtoa hoja aliendesha ushahidi wake akimtaja Kitany, lazima waziri pia ajibu madai hayo. 

Waziri wa Kilimo Mithika Linturi na wakili wake Muthomi Thiankolu Picha: EZEKIEL AMING'A
Waziri wa Kilimo Mithika Linturi na wakili wake Muthomi Thiankolu Picha: EZEKIEL AMING'A

Uhusiano wa awali kati ya Waziri wa Kilimo Mithika Linturi na Mbunge wa Aldai Maryanne Kitany ulichukua nafasi kubwa katika kikao cha kamati ya bunge inayosikiza tuhuma dhidi ya waziri Linturi siku ya Alhamisi.  

Wanachama wa Kamati Teule kuhusu Pendekezo la Kufutwa kazi kwa Linturi walitofautiana vikali iwapo walihitaji kupewa maelezo kuhusu uhusiano wa siku za nyuma wa wawili hao.  

Mwakilishi wa Wanawake wa Busia Catherine Omanyo aliiomba kamati hiyo kumwalika Kitany kufika mbele ya kamati ili kutoa maelezo yake kuhusu tuhuma dhidi ya waziri.  

 "Ingawa tunasikiliza upande wa waziri, mtu anayetajwa hayuko hapa kujitetea na ndiyo sababu tunapata ugumu kuendelea. Hatuwezi kusikiliza upande mmoja wakati upande mwingine haupo. Acha mbunge aje kujitetea,” Omanyo alisema.  

Mwenyekiti wa kamati Naomi Waqo alisema ataamua iwapo atamwalika Kitany baadaye.  

“Omanyo ameomba kwamba tumwalike Kitany. Tutashughulikia suala hilo wakati mwiingine baadaye,” Waqo alisema.  

Waqo alibainisha kuwa kamati hiyo haikumzuia mwasilishaji wa hoja hiyo Mbunge wa Bumula Jack Wamboka kuwasilisha kesi yake.  

“Najua kujadili mambo ya chumbani si rahisi, lakini tumewekwa katika hali hii na mtoa hoja. Sasa kwa kuwa hawakuiondoa, inabidi tuendelee. Waziri yuko huru kujibu,” Waqo aliongeza.  

Aliongeza kuwa umma ulimsikia Wamboka Jumatano, na sasa wanafaa kusikia upande wa Linturi.  Mbunge wa Tharaka Gitonga Murugara alisema inasikitisha kwamba kamati hiyo imelazimika kushughulikia masuala yaliyowasilishwa na mwasilishaji wa hoja ya kuondolewa kwa waziri.  

"Kesi za korti zilianzishwa na mtoa hoja kwa hivyo lazima Waziri ajibu," alisema.  

Mbunge wa Matuga Kassim Tandaza alibainisha kuwa kwa sababu mtoa hoja aliendesha ushahidi wake akimtaja Kitany, lazima waziri pia ajibu madai hayo.  

"Sioni chochote kibaya isipokuwa wanazungumza juu ya mambo zaidi ya hati za kiapo," alisema.  

Akitoa maoni yake siku ya Jumatano, Wamboka aliambia Linturi kutomuingiza Mbunge wa Aldai katika sakata ya kung'atuliwa kwake.  

Wamboka alisema inasikitisha kwamba Waziri alimtaja mbunge huyo katika barua yake ya majibu.  

Wamboka alisema ilikuwa ni bahati mbaya kwa Waziri huyo kuendelea kumvuta Kitanyi katika kila jambo ilhali ana familia yake.

Imetafsiriwa na Davis Ojiambo.