Familia ya Mkenya aliyefariki kwenye Mlima Everest yavunja kimya, yaeleza kilichotokea

"Sote tumehuzunishwa na yaliyompata ndugu yetu Cheruiyot Kirui kwenye Mlima Everest," familia ya Cheruiyot ilisema.

Muhtasari

•Walisema marehemu pamoja na mwenzake Nawang Sherpa walipoteza mawasiliano na kambi ya chini kabla ya wote wawili kuanguka.

•Familia hiyo pia ilituma risala za rambirambi kwa familia ya mwenzake Cheruiyot Nawang Sherpa ambaye bado hajapatikana.

akipumua kwa umbali wa mita 6,000 kwenye Mlima Manaslu, Nepal, mwaka jana.
Cheruiyot Kirui akipumua kwa umbali wa mita 6,000 kwenye Mlima Manaslu, Nepal, mwaka jana.
Image: HISANI

Familia ya marehemu mpanda milima wa Kenya Cheruiyot Kirui aliyefariki kwenye Mlima Everest nchini Nepal ilijitokeza siku ya Ijumaa kuzungumzia kilichojiri.

Marehemu mfanyakazi huyo wa Benki ya KCB alifariki akiwa katika harakati hatari ya kujaribu kupanda mlima mrefu zaidi duniani bila oksijeni ya ziada.

Katika taarifa siku ya Ijumaa, familia ya Cheruiyot ilieleza masikitiko yao kufuatia kufariki kwa mmoja wao.

Walithibitisha kwamba marehemu pamoja na muongozi wake Nawang Sherpa walipoteza mawasiliano na kambi ya chini kabla ya wote wawili kuanguka.

"Sote tumehuzunishwa na yaliyompata ndugu yetu Cheruiyot Kirui kwenye Mlima Everest," familia ya Cheruiyot ilisema kwenye taarifa.

"Cheruiyot alipoteza mawasiliano ya redio na kambi yake mapema asubuhi ya Mei 22, 2024 katika harakati zake za kukwea hadi kilele. Aliripotiwa kutoweka na mwenzake katika msafara na mara moja timu ya waokoaji waliokuwa kwenye kambi ya 4 walitumwa hadi kufikia hatua ya kuwasiliana mara ya mwisho.

Mwili wake uligunduliwa kwenye mwinuko wa mita 8,800, mita 48 kutoka kwenye kilele. Ingawa haiwezekani kubainisha matukio yaliyojiri kikamilifu, tunajua kwamba Cheruiyot na muongozi wake wa sherpa, Nawang Sherpa, walianguka,” taarifa hiyo ilisoma zaidi.

Familia hiyo pia ilituma risala za rambirambi kwa familia ya mwenzake Cheruiyot Nawang Sherpa ambaye bado hajapatikana.

“Taarifa zaidi zitatolewa kwa wakati ufaao. Asante na Mungu akubariki,” walisema.

Cheruiyot ambaye alitoweka alipokuwa akijaribu kupanda Mlima Everest  bila oksejeni ya ziada alipatikana amefariki siku ya Alhamisi.

Everest Today iliripoti kuwa mwili wa Cheruiyot ulipatikana mita chache chini ya kilele cha Mlima Everest.

Marehemu alikuwa kwenye safari hatari ya kupanda mlima bila oksijeni ya ziada akiwa pamoja na mpandaji mwenzake Nawang Sherpa kutoka Nepal ambaye alitoweka naye.

“Kwa huzuni kubwa, tunatoa habari za mpanda milima Mkenya Cheruiyot Kirui kufariki dunia kwenye Mlima Everest. Mwili wake ulipatikana mita chache chini ya kilele cha Mt Everest," Everest Today iliripoti kupitia Twitter.

"Alikuwa kwenye safari ya kuthubutu kufika kileleni bila oksijeni ya ziada na aliandamana na mpanda milima wa Nepal Nawang Sherpa, ambaye hatima yake bado haijulikani (alitoweka naye). Nia yake isiyoweza kuepukika na shauku yake ya kupanda mlima itakuwa msukumo milele. Tunatuma salamu zetu za rambirambi kwa familia na marafiki zake katika kipindi hiki cha majonzi. Pumzika kwa amani, Cheruiyot,” ripoti iliongeza.

Cheruiyot alikuwa mfanyakazi wa benki. Alikuwa amepanda hadi kilele cha  Mlima Kenya, mara 15.